Simba, Singida BS zaidi ya fainali leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:03 AM Dec 28 2024
Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Picha:Simba
Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

ITAKUWA ni patashika nguo kuchanika kwa wenyeji Singida Black Stars FC kuwakaribisha vinara, Simba katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani, Singida.

Hiyo ni moja ya mechi zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini msimu huu na kuifananisha na mchezo wenye hadhi ya fainali.

Ushindi ndio matokeo pekee yatakayowafanya Simba kuendelea kukaa kileleni na kula sikukuu ya Mwaka Mpya  2025 wakiwa wanaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kocha Mkuu, Fadlu Davids, amekiri  haitakuwa mechi rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao.

"Tunakwenda kucheza na timu nzuri, yenye wachezaji wazuri, lakini tumejiandaa  kucheza na timu hiyo ili kuendeleza rekodi yetu," alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo atawakosa, Joshua Mutale, ambaye amebaki Dar es Salaam, pamoja na Valentine Nouma, ambaye amekwenda kufunga ndoa nchini kwao, Burkina Faso.

Aliongeza mchezaji wake mpya winga, Ellie Mpanzu, bado hajakuwa na uwezo wa kucheza dakika zote 90, ndiyo maana amekuwa hamchezeshi dakika nyingi.

"Najua wengi wanataka kumwona Mpanzu dakika zote 90, ni kweli hata sisi tunataka kwa sababu tunajua ana vitu vingi vya kutupa ambavyo anavyo, lakini hajacheza kwa muda mrefu, hivyo hayuko fiti kucheza kwa dakika zote, taratibu anapata utimamu wa mwili na watu watamfaidi," alisema kocha huyo.

Naye kiungo wa timu hiyo, Awesu Awesu, amesema inapokuja mechi ambayo Simba wanacheza hasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, inakuwa ngumu na haijalishi timu wanayocheza nayo.

"Ni mchezo mgumu na siyo huu tu, huwa nasema siku zote kila Simba inapocheza haijalishi na Singida Black Stars, mechi zake zinakuwa ngumu, lakini itakuwa ngumu kwa sababu ina wachezaji wenye viwango vya hali ya juu," alisema kiungo mshambuliaji huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alilimbia gazeti hili mechi ya leo kwao ni muhimu kwa sababu mbili, kwanza wanataka kumaliza mwaka na kuingia mpya wakiwa kileleni katika msimamo wa ligi, lakini kumaliza 2024, kwa ushindi.

"Haiwezekani tumalize mwaka kwa kufungwa, tunataka tuuage mwaka huu kwa kuwapa zawadi ya ushindi mashabiki wetu, pia tunataka kuingia mwaka 2025 kwa furaha," alisema Ahmed.

Simba itaingia uwanjani ikikumbuka iko kileleni kwa tofauti na pointi moja tu dhidi na mpinzani na bingwa mtetezi, Yanga yenye pointi 36.

Wakati huo huo, taarifa za ndani kutoka  Simba zinasema, Mutale ameomba kuondoka katika kikosi hicho, akitaka kutolewa kwa mkopo kwenye klabu ambayo atakwenda kucheza bila presha na kuboresha kiwango chake.

Inaelezwa viongozi wa Simba kwa sasa wapo katika mchakato huo wa kuangalia ni wapi mchezaji huyo anaweza kupelekwa nje ya nchi.

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhani, amesema wamejiandaa kucheza kutokana na ubora wa wapinzani wao.

"Tumejiandaa kutokana na ubora wa Simba, najua watakuja na maswali mengi ya kutuuliza, na sisi pia tutawapa maswali, itakuwa mechi kubwa, nzuri, inayohitaji umakini mkubwa kwa wachezaji, timu zote mbili zina wachezaji bora wenye uwezo wa hali ya juu, hivyo itakuwa mechi bora na ya kuvutia," kocha huyo alisema.

Singida Black Stars ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 33 kibindoni.

Baada ya mechi hiyo, Simba itarejea Dar es Salaam kuanza maandalizi ya kuelekea Tunisia kuwafuta, CS Sfaxien kwa ajili ya mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Januari 5, mwakani.