STRAIKA wa Singida Black Stars raia wa Kenya, Elvis Rupia, ambaye anawaniwa na klabu ya Simba kwa ajili ya kumsajili kwenye dirisha dogo la usajili, juzi alifunga mabao mawili na kukaa juu ya kilele cha orodha ya wafungaji wa mabao mengi Ligi Kuu, akifikisha mabao saba.
Kwenye Uwanja wa Liti, Singida, straika huyo mwenye mbio na nguvu pamoja na mashuti makali, alifunga mabao yote mawili yaliyoiwezesha timu yake ya Singida Black Stars kushinda mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji.
Alipachika mabao hayo dakika ya nane, na 15, kabla ya Yassin Mgaza kuifungia Dodoma Jiji bao la kufutia machozi, dakika ya 58.
Mabao hayo yamemfanya sasa kuongoza kwenye ufungaji Ligi Kuu, akimpiku kinara wa muda mrefu, Selemani Mwalimu wa Fountain Gate aliyebakiwa na mabao sita.
Matokeo hayo yanaifanya Singida Black Stars kufikisha pointi 27 sawa na Yanga, lakini ikiendelea kuwa nafasi ya nne kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Dodoma Jiji ikisalia na pointi 16, kwenye nafasi ya 10 kwenye msimamo.
Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhan Nswanzurimo, alisema ilikuwa ni mechi nzuri na ya kimbinu.
"Ilikuwa mechi ya kimbinu, kocha mmoja akibadili mfumo mwingine anabadilika, kipindi cha kwanza tulitawala mchezo, cha pili hatukuwa vizuri kwa sababu wachezaji wangu walionekana kujiamini kupita kiasi, ilionekana kama wamechoka kimwili, muhimu tumepata pointi tatu, bado tuna kazi ya kufanya," alisema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Macky, Mexime, alisema waliiharibu mechi dakika 20 za mwanzo ambapo hawakuwa makini na kuweza kutoa mwanya kwa wapinzani wao kufunga mabao yote mawili.
"Mechi tuliiharibu dakika 20 za mwanzo, hatukuwa makini tukawapa mabao rahisi, makosa mawili wakayatumia, kipindi cha pili tukaamka usingizini tukaitawala mechi lakini tukapata bao moja tu. Niseme tu walituhukumu kutokana na ubora wa wachezaji wao," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED