Mukoko: Yanga bingwa tena 2024/2025

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:18 AM Jun 17 2024
news
Picha: Mtandao
Mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga, Mukoko Tonombe.

MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Yanga, Mukoko Tonombe, ameitabiria timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kama itaendelea kuwa na asilimia kubwa ya wachezaji waliokuwa nao msimu uliomalizika.

Tonombe alisema kuwa klabu hiyo kwa sasa inatakiwa kuongeza tu baadhi ya wachezaji wachache wenye ubora kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Tonombe, aliyeichezea Yanga kuanzia 2020 hadi 2022, amesema wala hatoshangaa kuiona timu hiyo ikifika fainali msimu ujao kama itaendelea kuwa na kina Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Yao Kouassi, Djigui Diarra, Pacome Zouzoua na wengine ambao itawaongeza watakaokuwa nsa ubora zaidi.

Alisema kwa sasa Yanga ina wachezaji wengi bora zaidi kuliko walivyokuwa wao ndani ya kikosi hicho.

"Nimeona timu yangu ya zamani, wamechukua wachezaji wenye viwango vikubwa zaidi, walisajili wazoefu wa michezo ya kimataifa ndiyo maana wamewasaidia kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na hili lilikuwa jambo bora zaidi.

Kama wataendelea na asilimia kubwa ya wachezaji hawa wa msimu uliopita, na wakaongeza wengine ambao wana viwango sawa nao au kuzidi, naiona msimu ujao ikifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wala haina shaka kabisa," alisema mchezaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Yanga ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika, ikatolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju 3-2 ya penalti, baada ya timu hizo kucheza mechi nyumbani na ugenini bila kufungana ndani ya dakika 90.

Akizungumza kuhusu soka la Tanzania, Tonombe alisema kwa sasa limekua sana, huku akikiri kuumizwa mno alipoachwa na klabu ya Yanga, 2022.

Nimemisi sana maisha ya soka la Tanzania, nilivyoondoka Yanga niliumia sana, sababu kubwa ni kwamba mashabiki wa hapa wanapenda sana mpira, pili ni sehemu nzuri tulivu na ndiyo maana nimekuja tena hapa nchini," alisema.

Kiungo huyo mkabaji alisema kwa sasa amemaliza mkataba na TP Mazembe, na ana ofa nyingi mkononi, na muda si mrefu mashabiki wote watajua anaelekea wapi.

"Maisha ndivyo yalivyo, nimecheza Yanga nimetoka hapa, nimekwenda TP Mazembe, kwa sasa kule mkataba wangu umeisha, nimekuja Tanzania kuangalia marafiki zangu, familia ya mke wangu na Watanzania kwa ujumla.

Ni kweli nina ofa nyingi sana, utaona tu pale nitakapotua msimu ujao, nilimisi sana maisha ya Tanzania, kwangu naona mazuri mno," alisema mchezaji huyo.