Ligi Kuu Z'bar yazidi kunoga

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 11:06 AM Oct 21 2024
KVZ FC.
Picha: Mtandao
KVZ FC.

VITA ya ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar imezidi kupamba moto huku kukiwa hakuna mbabe ambaye amepata ushindi kwa asilimia 100.

Timu ambazo hazijaonja machungu ya kupoteza hadi sasa ni nne tu, ambazo ni KVZ FC, Mlandege FC, Malindi SC na Chipukizi FC, lakini hazijashinda kwa asilimia 100, kwani zote kuna mechi zimebanwa mbavu kwa kulazimisha ama kulazimishwa sare.

Ligi hiyo inajumuisha timu 16 ambapo mwisho wa msimu, nne kutoka mkiani katika msimamo wa ligi hiyo, zitashuka daraja kwa kurudi Ligi Daraja la Kwanza kwa Kanda walizotoka, Unguja na Pambe.

Hadi kufukia sasa ligi hiyo ipo  mzunguko wa saba, huku timu ya Inter Zanzibar FC ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja katika michezo saba aliyocheza.

Timu ya pili kutoka mkiani ni Tekeleza FC nayo ina alama moja ikiwa imecheza michezo sita, ikifuatiwa na New City FC ambayo ina pointi mbili katika michezo saba na ya nne kutoka chini ni Mwenge SC ambayo ina alama nne katika michezo saba.

Kwa upande wa timu nne za juu ni Mwembe Makumbi City ndio kinara wa ligi hiyo ikiwa na alama 15, nafasi ya pili ikikaliwa na  KMKM SC yenye pointi 14 ikifuatiwa na Mafunzo FC wenye alama 13 sawa na Malindi inayoshika nafasi ya nne.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Issa Kassim, alisema kwa kiasi yapo makosa kadhaa ambayo yalijiyokeza katika mizunguko iliyopita kwa waamuzi na baadhi ya viongozi wa timu na wamechukuliwa hatua.

Alisema bodi hiyo imekuwa ikifanya tathimini kwa kila mzunguko ili kuchukua hutua kwa mambo ambayo yanajitokeza ambayo ni kinyume cha kanuni za ligi hiyo.

Hata hivyo, alisema Bodi ya Ligi itaendelea kufanya hivyo ili kupunguza au kuondosha kabisa vitendo vyote vinavyokwenda kinyume cha kanuni, iwe kwa waamuzi au klabu.