KenGold yaanza mipango mapema

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 06:18 AM May 04 2024
Mkurugenzi wa KenGold, Keneth Mwambungu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa KenGold, Keneth Mwambungu.

BAADA ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa klabu ya KenGold ni kama wameshtuka kwa kujipanga kuanza mipango ya usajili mapema ili kujiweka imara.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa KenGold, Keneth Mwambungu, amesema wametumia nguvu kubwa na kupambana kupanda daraja, hivyo hawataki kuona wanashuka haraka au kushiriki Ligi Kuu kwa msimu mmoja.

Mwambungu alisema wameanza mikakati ya kukiimarisha kikosi chao ili kutoa ushindani katika kila mechi ya Ligi Kuu watakayocheza.

"Ni ngumu kusema tutachukua ubingwa msimu wa kwanza tu wa Ligi Kuu, lakini tunataka kuonyesha ushindani na hata mwishoni mwa ligi tuwe na uhakika wa kuendelea kubakia," alisema Mwambungu.

Aliongeza licha ya kuwa na kikosi kizuri ambacho kimewapandisha daraja, wamepanga kukiimarisha zaidi pamoja na benchi la ufundi hili kwenda na kasi ya Ligi Kuu.