Fadlu : Tungewachapa nyingi

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:39 AM Sep 28 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kama isingekuwa uchovu, timu yake ingepata ushindi mnono zaidi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar juzi usiku.

Katika mchezo huo Simba ikiwa ugenini ilipata ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa Leonel Ateba na Fabrice Ngoma na kufikisha pointi tisa.

Simba imekutana na Azam FC ikiwa zimepita siku chache baada ya kumaliza mechi mbili ngumu za kimataifa za mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli kutoka Libya.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi hiyo kumalizika, Fadlu alisema wachezaji wake walikuwa na uchovu wa michezo hiyo miwili ya kimataifa pamoja na kusafiri umbali mrefu na kama si hali hiyo, basi wangepata ushindi mkubwa zaidi hapo juzi.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini alisema mechi mbili za CAF wakianzia ugenini Libya na marudiano hapa nchini zimewachosha wachezaji wake huku wakilazimika kucheza mechi nyingine ngumu ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC baada ya siku tatu.

Kocha huyo aliongeza kama wachezaji wake wangepata mapumziko sawasawa kabla ya mechi hiyo, ana uhakika wangeshinda mabao mengi zaidi.

"Nimefurahi kushinda dabi hii, lakini ukweli kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri sana kwetu, tuliwakaba vizuri, tuliiba mipira mingi kutoka kwa wapinzani wetu na kuwasababishia hatari, tungeweza kupata zaidi ya bao moja.

Nadhani haikuwa hivyo sana kipindi cha pili kwa sababu ya mfululizo wa mechi, tumecheza mechi tatu kwa muda mfupi sana, michezo miwili dhidi ya Al Ahli Tripoli, tumesafiri umbali mrefu mno, vinginevyo leo (juzi), hadithi ingekuwa nyingine, tungeweza kushinda mabao mengi," alisema Fadlu.

Aliongeza na kama wachezaji wake wangetumia vyema nafasi walizotengeneza, walistahili kuimaliza mechi hiyo katika dakika 45 za kwanza.

Alisema alilazimika kufanya baadhi ya mabadiliko kipindi cha pili ambayo si ya kiufundi bali ya kuwapumzisha wachezaji wake kwa ajili ya mchezo mwingine utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma wenyeji dhidi ya Dodoma Jiji FC.

"Nilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa ajili ya kupumzisha baadhi ya wachezaji kwa ajili ya mchezo wetu mwingine wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumapili. Hakuna muda wa kupumzika, hakuna muda wa kufanya mazoezi. Nawashukuru sana wachezaji wangu, pamoja na uchovu bado wameendelea kupambana na kuipa timu ushindi," aliongeza kocha huyo.

Alimpongeza kipa wake, Mussa Camara, kwa kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa mechi ingawa hakuokoa mashambulizi ya hatari.

Naye Kocha Mkuu wa Azam, Rachid Taoussi, alisema wachezaji wake walicheza vyema mchezo huo, lakini wameangushwa na maamuzi mabaya ya waamuzi.

Taoussi alisema timu yake ilitawala mchezo lakini walikosa ushindi huku akiongeza mabao yote mawili ya Simba yalikuwa yakuotea.

"Nimechukizwa sana, sababu mmeona, tumecheza vizuri sana, lakini naona kama mabao yote mawili yalikuwa ya kuotea na tunahitaji VAR kwa ajili ya kutafsiri matukio kama haya," alilalamika kocha huyo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba iko katika nafasi ya tatu huku Azam iliyopoteza kwa mara ya kwanza msimu huu ikifuatia ikiwa na pointi nane kibindoni baada ya kucheza michezo mitano.