Dewji ambakisha Ayoub Simba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:23 AM Jun 17 2024
news
Picha: Simba sc
Golikipa namba moja wa Simba Sc, Ayoub Lakred.

MWEKEZAJI, Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohamed Dewji, amefanikiwa kumbakisha golikipa namba moja wa timu hiyo kwa sasa, Ayoub Lakred kwa kumwongezea mkataba wa mwaka mmoja.

Taarifa za uhakika zilizopatikana jana zinasema kuwa kipa huyo ambaye tayari alikuwa amemaliza mkataba wake wa msimu mmoja na hakutaka kuendelea tena na timu, amebadili mawazo baada ya mazungumzo ya kina na Mo mwenyewe ambaye amemshawishi hadi kufikia hatua hiyo.

"Ayoub amebaki, juzi amesaini tena mkataba wa mwaka mmoja, sasa anakaa hadi Juni 2025, bosi Mo ndiye aliyembadili mawazo. Hakutaka tena kuendelea kuitumikia Simba, kuna klabu kadhaa Misri, kwao Morocco na Tunisia zilikuwa zinamhitaji, ikiwamo FAR Rabat ambako alitoka, kwa hiyo bado tunaye," kilisema chanzo chetu ndani ya klabu hiyo.

Alisema mazungumzo hayo yalifanyika kwa njia ya simu, na si kwamba alikwenda Dubai, Falme za Kiarabu kukutana na Mo kama inavyozunguzwa.

Mtoa taarifa huyo alisema kwa sasa Ayoub yuko nchini kwao Morocco akipumzika na familia yake.

Kipa huyo alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu uliopita, ambapo hakuwa na wakati mzuri mwanzoni, mashabiki wa timu hiyo wakiona kama hawakupata mtu sahihi wa kushindana na Aishi Manula, lakini muda mchache alibadilika baada ya kile kinachoelezwa kuzoea hali ya hewa na mazingira, akawa kwenye kiwango cha hali ya juu na kushangaza wengi.

Hadi Ligi Kuu msimu uliomalizika unafikia ukingoni, alikuwa ndiye kipa namba moja wa timu hiyo, ambapo nafasi hiyo hauikuja hivi hivi bali kazi kubwa aliyokuwa akiifanya ya kuokoa michomo ya hatari kutoka kwa wapinzani waliokuwa wakicheza dhidi ya timu hiyo, hasa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Hatukuwa vizuri msimu uliomalizika, lakini kipa huyu alitusaidia sana, alikuwa na kiwango kikubwa mno, aliangushwa na safu ya ulinzi, kiungo mkabaji, na timu nzima kwa ujumla, sasa kwa usajili huu unaoendelea nafikiri atakuwa kwenye kiwango bora zaidi kuliko hata cha msimu uliopita," kilisema chanzo hicho.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania, Mei 28, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Ayoub alionekana kuwaaga mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa wamekaa jukwaani na kutoa ishara kuwa anaondoka ndani ya klabu hiyo.