Coastal Union kumpima Shaban Kagame

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:30 AM Jun 17 2024
Klabu ya Coastal Union.
Picha: Mtandao
Klabu ya Coastal Union.

UONGOZI wa klabu ya Coastal Union umepanga kutumia mashindano ya Kagame Cup yatakayofanyika hivi karibuni kama maandalizi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika huku pia wakitumia kumpima beki Djuma Shaaban.

Coastal tayari imefanya mazungumzo na mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na watampa mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliiambia Nipashe kuwa wamefurahia kushiriki michuano ya Kagame msimu huu kwa kuwa yatakuwa sehemu ya maandalizi yao kabla ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

"Tumeyapokea mashindano hayo kwa fikra chanya, kwetu sisi itakuwa sehemu ya maandalizi ya michuano ya CAF, tutapata mechi za kimataifa kujipima," alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutwajwa jina lake.

Aidha, alisema tayari wameshamalizana na Djuma lakini watayatumia mshindano hayo ya Kagame kama kipimo kwake kuona kama atawasaidia.

"Kila kitu kipo sawa, tumeshakubaliana naye, lakini mashindano ya Kagame ni kipimo kwake kuona nini ambacho atakiongoza kwenye kikosi chetu," alisema kiongozi huyo.

Coastal Union itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza Ligi Kuu ikiwa kwenye nafasi ya nne nyuma ya wawikilishi wenza, Simba.