ILI kupoza maumivu ya kutolewa kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Yanga umesema kikosi chao kimejipanga kutoa vipigo katika kila mechi watakayocheza wakianza na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Copco FC utakaochezwa kesho, imeelezwa.
Yanga inatarajia kuikaribisha Copco katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA itakayochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema si wanachama, mashabiki na viongozi wa timu hiyo pekee ndio waliohuzunika baada ya kutolewa katika mashindano ya kimataifa, bali hata wachezaji pia waliumia.
Kamwe alisema ili kuendelea upya na safari ya kutetea ubingwa wa FA na Ligi Kuu Tanzania Bara, wachezaji wa Yanga wameahidi kuwafuta machozi kwa kushinda michezo inayofuata.
"Nilikaa na wachezaji wetu nikawaambia wangeonyesha angalau asilimia 60 tu ya uwezo walioonyesha katika mechi dhidi ya Al Hilal iliyochezwa Mauritania, basi mechi ile na MC Alger tungeshinda, lakini ndiyo mpira, leo wanaweza kulala vizuri na kuamka vibaya.
Hata wao wamehuzunika, wamenihakikishia hasira zao watazirudisha katika Ligi Kuu wakianza kesho dhidi ya Copco, tunawaomba wanachama na mashabiki wa Yanga waendelee kutuunga mkopo na kuwa nyuma ya wachezaji wetu kila mechi wajitokeze kwa wingi uwanjani," alisema Kamwe.
Wakati huo huo wachezaji wa zamani wa Yanga wamejitokeza kuelezea kilichosababisha timu hiyo kutolewa ni wachezaji kuwa wazito.
Stephano Mwasika, beki wa kushoto wa zamani wa timu hiyo, alisema katika mechi dhidi ya Waarabu, wachezaji wa Yanga walionekana wakicheza tofauti na walivyotegemewa.
"Tulionekana kucheza lakini hatukuonekana kutafuta ushindi tangu dakika ya kwanza, wachezaji walionekana wazito tofauti na watu walivyokuwa wakitegemea, sijui waliamka vipi, lakini timu nzima haikucheza vizuri. Nadhani kwa sasa kila mtu atulie kwa sababu tuna michezo ya Ligi Kuu na Kombe la FA, tunatakiwa kufanya vizuri pia," Mwasika, ambaye aliichezea Yanga kuanzia 2010, hadi 2013 akitokea Moro United alisema.
Aliyekuwa straika hatari wa timu hiyo kati ya mwaka 1990 na mapema mwaka 2000, Mohamed Hussein 'Mmachinga', aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kujua kuwa mpira una matokeo matatu hivyo wanatakiwa kutulia baada ya jambo hilo kutokea.
Mmachinga alisema utulivu pekee ndiyo utakaowafanya wachezaji na viongozi wapate nguvu ya kufanya vyema katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na FA na hatimaye kutetea mataji hayo.
"Mpira una matokeo matatu, ukiwa kama mwanamichezo ni lazima upokee matokeo yote, kikubwa ni kujipanga kuangalia tutafanya nini baadaye na kwa sababu tunarudi kwenye ligi, nguvu zetu sasa zote tuhamishie huko tupate ubingwa," alisema Mmachinga ambaye pia aliwahi kuicheza Simba.
Yanga ilianza na mguu mbaya katika mechi za hatua ya makundi baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan na kwenda kufungwa idadi kama hiyo ya magoli ugenini Algeria na wenyeji MC Alger.
Katika mechi ya mwisho, Yanga ikihitaji ushindi wowote ili isonge mbele, MC Alger wao walihitaji sare ya aina yoyote ili kutinga hatua ya robo fainali, na sare ya bila kufungana iliwabeba Waarabu hao.
Baada ya mchezo wa kesho, Yanga itawakaribisha Kagera Sugar katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Februari 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED