NYOTA ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo nchini imezidi kung'aa baada ya mabondia wa wazawa kufanya vizuri katika mapambano ya 'Knockout ya Mama' yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam juzi na kufanikiwa kuibakiza mikanda yote Tanzania.
Pambano hilo limewakutanisha mabondia kutoka Ufilipino, Burundi, Afrika Kusini, Nigeria na wenyeji Tanzania likiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia.
Rais Samia alinogesha patashika hiyo kwa kutoa bonasi ya Sh. milioni 10 kwa Watanzania watakaoshinda mikanda ya ubingwa kwa Knock Out (TKO) na Sh. milioni tano kwa wale watakaoshinda kwa pointi na Sh. milioni moja kwa wale ambao walitamba kwenye mapambano ya kimataifa yasiyokuwa ya ubingwa.
"Wosia wangu mchezo vizuri, sheria zifuatwe," alisema Rais Samia alipokuwa akizungumza na mashabiki na kuwataka mabondia kuiheshimisha nchi katika nyanya za kimataifa, kupitia sekta ya mchezo wa ngumi.
"Nimesikia kuna mabondia kutoka nje ya nchi, mabondia wetu Watanzania mpewe Bendera ya Taifa na muipiganie nchi yenu," alisisitiza Rais Samia.
Naye Waziri Mkuu, Majaliwa, alieleza namna mchezo wa ngumi unavyopendwa nchini na kusema ni mchezo wa tatu kupendwa baada ya soka na kikapu.
Mtanzania aliyefungua dimba la ubingwa ni Yohana Mchanja aliyetwaa ubingwa wa World Boxing Organisation Global Championship dhidi ya Miel Farjado kutoka Ufilipino huku Salmin Kassim akimchapa, Adrian Lerassan, wa Ufilipino kwa pointi 3-0 na kutwaa ubingwa wa Mabara.
Ibrahim Mafia alitwaa taji la WBC Afrika kwa kumchapa kwa pointi, Lusizo Manzana kutoka Afrika Kusini huku Said Chino akitetea Ubingwa wa Mabara wa IBA kwa kumchapa kwa pointi, Michael Klassen raia wa Afrika Kusini na Kalolo Amir alishinda kwa pointi dhidi ya Shile Jelwana wa Afrika kusini na kutwaa wa PST.
Katika mapambano mengine yasiyokuwa ya ubingwa, Maisha Samson alichapwa kwa TKO, sekunde ya 218 ya pambano dhidi ya Mtanzania mwenzake, Juma Thabiti huku Omari Omari akikutana na kipigo kama hicho kutoka kwa Shauri Athumani katika raundi ya tano na Luqman Kimoko alimchapa Bismark Saah wa Ghana kwa pointi.
Naye Leila Macho alimchapa Agnes Mtimaukanena wa Burundi kwa pointi wakati Fadhil Majiha alimwadhibu kwa pointi za majaji wote, John Zile kutoka Ghana na Mganda Latibu Muwonge alikalishwa kwa kipigo cha TKO na Abbada Cadabra dakika ya 2:22 wakati Abdulrahman Magoma akishinda kwa pointi dhidi ya Festus Simon.
Bondia raia wa India, Gurpreet Signh alipigwa kwa TKO dakika ya 1:50 na Said Bwanga baada ya kuumia mkono wa kulia ulingoni wakati Salim Mtango (Mesi wa ngumi) akikutana na zomea zomea ya mashabiki baada ya kutangazwa mshindi kwa pointi dhidi ya Azeez Lateef wa Nigeria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED