KATIKA Shule ya Msingi Kawe A, iliyopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kumejengwa mifumo na miundobinu inayowezesha shule hiyo kupata zaidi ya lita 6,000 maji kila siku kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine katika taasisi hiyo.
Miundobinu hiyo inajumuisha matanki manne yote kwa pamoja yakiwa na ujazo wa lita 1,000 ambazo ni kwa ajili ya huduma ya maji ya kunywa pekee kwa wanafunzi wa shule hiyo ambao ni zaidi ya 1,200.
Hata hivyo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Cuthbert Mfwangawo anasema lita 1,000 za maji ya kunywa ambazo hujazwa kwenye matanki hayo manne kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), hayatoshelezi mahitaji halisi kwani humalizika kwa siku moja.
"Mahitaji ya maji yameongezeka kutokana na joto kali, tunajitahidi kuhakikisha watoto wanapata maji ya kunywa, lakini changamoto za gharama na miundombinu zinatufanya tushindwe kufikia mahitaji yote,” anasema Mwalimu Mfwangawo.
Mwl. Mfwangawo anasema mahitaji halisi ya maji ya kunywa kwa siku katika Shule ya Msingi Kawe ‘A’ ni walau lita 1,500 hivyo kuna uhitaji wa matenki ya nyongeza ili kufikia kiwango kinachotosheleza idadi ya wanafunzi waliopo.
Kuhusu usafi na usalama wa maji hayo mwalimu huyo anasema: “shule yetu inatumia dawa aina ya ‘water guard’ kutibu maji, kila siku jioni.”
Mmoja wa wanafuni wa shule hiyo, Yerenus Ponela ambaye ni mwanachama wa klabu ya Mazingira ya Wakulima Chipukizi iliyopo shuleni hapo, anasema wanakabiliwa na ongezeko la joto kali, hali inayosababisha kutumia maji ya kunywa kwa wingi, ukilinganisha na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Anasema kwa sasa ana uwezo wa kunywa maji zaidi ya lita moja kwa siku akiwa shuleni ukilinganisha na kipindi cha awali ambapo alikuwa anakunywa maji kwa kiwango kidogo.
Klabu ya Wakulima Chipukizi imeanzishwa kupitia Mradi wa Pamoja Tudumishe Elimu unaotekelezwa shuleni Kawe ‘A’ kupitia ushrikiano wake na Shirika la WeWorld ambako wanafunzi wanafanya kazi za uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya kuwashirikisha katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Ongezeko la joto juu ya ardhi linatajwa kama matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo pia yana athari kubwa kwa watoto. Ripoti ya Shirika la kuhudumia Watoto Ulimwenguni (UNICEF) yenye jina la ‘The State of the World’s Children 2024’ inataja uhaba wa maji uwa miongoni mwa changamto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuleta athari kwa watoto na kundi la vijana balehe.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka 2024 athari nyingine ni ongezeko la magonjwa ya kuhara yanayotokana na mafuriko ambayo husababisha kujaa kwa mito, mifereji na mabwawa, hivyo maji husambaa kwenye makazi ya watu. “Magonjwa ya haya ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo kwa watoto walio chini ya miaka mitano,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Usafi wa mazingira
Kwa upande mwingine, shule ya Msingi Kawe ‘A’ ina kisima chenye ukubwa wa ujazo wa lita 5,000 za maji ambayo hutumika vyooni kupitia miundombinu iliyojengwa kwa msaada Shirika la We World.
Mfumo wa maji ya vyooni pia hupoke maji kutoka kwenye kisima hicho, yakiunganishwa na yale yatokayo DAWASA, hivyo kuwezesha watoto kunawa mikono mara baada ya kutoka maliwatoni ikiwa ni hatua ya kuwalinda dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mfwangawo, shule hiyo ina matundu 31ya vyoo yaliyounganishwa kwenye mfumo wa majitaka. Kati ya hayo, 22 ni vya wasichana na tisa ni wavulana.
Kuwapo umuhimu wa upatikanaji wa huduma za majisafi na majitaka, ni miongoni mwa masuala yanayotajwa katika maazimio ya mkutano wa watoto na vijana balehe 150 uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 2023.
Watoto na vijana hao, walioungana na wenzao zaidi ya 12,000 waliotoa maoni kupitia mpango ulioitwa ‘U survey’, ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi za Tanzania za Shirika la Watoto Ulimwenguni (UNICEF).
Maoni hayo yalikusanywa kati ya Julai na Oktoba 2023 kutoka kwa watoto na vijana balehe wa Kitanzania, na hatimaye kuwezesha kuandikwa kwa ripoti iliyobebba mtazamo wa jumla wa kundi hilo kuhusu linavyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti ya matokeo ya utafiti huo jumuishi inayoitwa “Children for Climate Action:
Voices from Tanzania” kwa tafsiri isiyo rasmi (Hatua za watoto na mabadiliko ya tabianchi: Sauti kutoka Tanzania), inataja masuala kadhaa ambayo kundi hilo linayaona kuwa changamoto katika makuzi na maendeleo yake.
Miongozi mwa changamoto hizo ni uhaba wa maji ambao husababishwa na ukame katika maeneo kadhaa, joto kali kuliko kawaida na ufyekaji holela wa misitu. Wanasema hali hiyo inawanyima haki zao za msingi, ikiwemo ya ulinzi hasa katika maeneo ya vijijini wanakofuata huduma husika mbali ambako wanahatarisha maisha yao.
Katika mapendekezo yao, wanasema: “Watoto na vijana-balehe wanatoa wito kwa serikali na wadau wake wa maendeleo kuchukua hatua za kuwezesha upatikanji wa maji katika maeneo yanayofikika ili kuwalinda dhidi ya vitendo uonevu na unyanyasaji.”
Ushirikishwaji wa watoto
Utafiti wa U-Report unasema asilimia 60 ya watoto na vijana waliohojiwa walisema hawajifunzi vya kutosha kuhusu changamoto za tabianchi wakiwa shuleni huku asilimia 80 wakisema mafunzo hayo ni muhimu kwa mustakabali wao wa siku zijazo.
Katika moja ya maanzimio yaliyoko kwenye ripoti hiyo (U-Report), kundi hilo linapendekeza suala ya mabadiliko ya tabianchi kuwa sehemu ya mtaala wa elimu. “Tunapendekeza mada za tabianchi katika mafunzo yanayotumia sanaa, kama vile nyimbo za kuelimisha masuala ya hayo, ili kuongeza ufahamu wa kila siku kuhusu uwajibikaji wa kimazingira,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Shule Kawe ‘A’ hoja hiyo ni kama imeanza kupata majawabu kwani Mwalimu Mfwangawo anasema katika kukabiliana na ongezeko la joto kali, wanafuta suluhu ya kwa njia ya ushirikishwaji wakianza kuwafundisha wanafunzi namna ya kuhifadhi na kutunza mazingira.
Anasema ushirikishwaji huo unafanyika kupitia Mradi wa Pamoja Tudumishe Elimu unaotekelezwa kwa kushirikiana na WeWorld, lengo likiwa ni kuwasaidia watoto kupata elimu ya vitendo ili waweze kukabiliana na changamoto za mazingira wanapokuwa shuleni na hata wakiwa nyumbani.
“Watoto wamefundishwa kulima mboga kama mchicha, nyanya, na maboga. Kilimo hicho huchangia siyo tu lishe bora, bali pia huimarisha afya zao kwa kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama pumu na saratani ya ngozi,” anasema Mwalimu.
Mwanafunzi wa darasa la tano, katika shule hiyo Kawe ‘A’, Mulhat Majid Issa ambaye pia ni mwanachama wa Klabu ya Mazingira ya Wakulima Chipukizi, anasema walimu wamewafundisha umuhimu wa kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mulhat anasema, elimu hiyo wanaifanya kwa vitendo wakilima bustani za mboga, matunda na upandaji miti na inawasaidia kutambua umuhimu wake kwa mustakabali wa maisha yao ya baadaye.
Klabu za mazingira
Pendekezo jingine ambalo lilitokana U-Report ni kuanzishwa kwa klabu za mazingira katika shule za msingi na sekondari. “Serikali inapaswa kuanzisha vilabu mbalimbali katika shule za msingi na sekondari na kwenye jamii ili kukuza uhifadhi wa mazingira,” ananukuliwa binti aitwaye Agnes (16) wa mkoani Mbeya.
Suala hilo pia ni kama limepatiwa jawabu kupitia Mradi wa Pamoja Tudumishe Elimu unaotekelezwa shuleni Kawe ‘A’ kupitia ushrikiano wake na Shirika la WeWorld ambako wanafunzi wanafanya kazi za uhifadhi wa mazingira kupitia Klabu ya Wakulima Chipukizi.
Mwalimu Mfwangawo anasema kupitia program ya upandaji miti inayofanyewa kwa kushirikiana na wanafunzi wanaounda klabu hiyo, miti 60 tayari imepandwa kuzunguka maeneo ya shule, ikiwa ni hatua ya kupunguza ukame na kuhifadhi uoto wa asili.
“Lengo la shule yetu ni kupanda miti 50 zaidi, hasa ya matunda, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata kivuli na lishe bora, kupitia juhudi hizo, watoto wanajifunza umuhimu wa mazingira na jinsi ya kuyatunza.” anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED