Simulizi ya Mwenyekiti wa Wagumba alivyotaka kuiba mtoto, akashindwa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:43 AM Sep 26 2024
Shamila Makwenjula, Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania (CCWTZ).
Picha: Mtandao
Shamila Makwenjula, Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania (CCWTZ).

SHAMILA Makwenjula, kwake hali ya ugumba inamfanya atafsiri dhana tofauti kwenye jamii, anapokabili hali anayoishi nayo kutokuwa na mtoto.

Hatua za unyanyapaa, kutodumu katika ndoa mbili alizopitia, kumemsababishia hisia kali na hata kuthubutu jaribio la kuiba mtoto.

Mzaliwa huyo wa mwaka 1973 katika kijiji cha Mtimbila, mkoani Morogoro, ameisimulia Nipashe wastani wa wiki mbili sasa, baada ya huduma ya upandikizaji mimba (IVF) kuzinduliwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Shamila kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania (CCWTZ), wazo lililoanza mwaka 2015, ila usajili na shughuli rasmi zilianza mwaka 2022, jumla ya wanachama sasa ni 600.

Anaueleza umoja wao ni mkusanyiko wa kinamama na kinababa wenye tatizo la ugumba na tasa, ajenda yao na kubadilishana mawazo na kupeana moyo, katika kulikabili tatizo lao kijamii na kitaifa.

Shamila anaeleza wanachama wengi ni wagumba ambao wanatibika, ila walio tasa hawatibiki kisayansi. 

SHAMILA NI NANI

Huyo pia ni mjasiriamali, anayesimulia maisha yake aliolewa akiwa na umri wa miaka 23 na baada ya miaka mitatu akaachika. Mwaka 1995, akaolewa tena na kudumu katika ndoa miaka 11 hadi mwaka 2006, akaachika tena.

 “Kuna mwaka nikiwa Dar es Salaam akili ilinituma niibe mtoto. Niliondoka kijijini, nikasema kwa kipindi cha miezi tisa hadi nitakaporudi watajuwa nilikuwa mjamzito, kumbe kwa muda huo nilipanga kuiba mtoto,” anasema.

Hata hivyo, anasema alikwamishwa na mambo makuu mawili; alishindwa kupata mtoto wa kuiba katika kipindi anajifanya na ujauzito miezi tisa, pia baadaye ikamjia hisia za kibinadamu namna angemtesa mwenye mtoto kisaikolojia.

 Shamila anaisimulia Nipashe, kwa muda mrefu hamu yake kuitwa ‘mama’ haijamtoka hasa alipokuwa kwenye ndoa na amefanya malezi ya watoto wa nduguze kama mbadala apate mtazamo chanya kwenye jamii, lakini bado azma yake kuwa mlezi halisi wa kudumu haikutimia.

“Ukiwa na mtoto, kwanza katika familia au jamii ni kama heshima fulani. Wagumba tunapata hisia kali sana na hata msongo wa mawazo, watoto ni faraja. 

“Wakati mwingine ukiwa nao ni ulinzi kwa familia ulikoolewa. Ebu fikiria umeolewa nyumbani hakuna watoto, mawifi, mama mkwe sijui wanakuonaje? 

“Hata urithi utaachiwaje na mume, familia ulikoolewa wanakuona huna mchango wowote, ndio maana kuna kesi nyingi za mali kuhusu wanandoa,” anasema Shamila. Hata hivyo, kisheria, kuna haki za msingi za mke.

 Mama huyo analalamika: “Tunaonekana hatujakamilika, wenye laana, mikosi, manyanyaso kama nilivyosema, ukiwa mke mwenza ndio usiseme! Ndio maana nikapata wazo la kuiba mtoto, hii sio siri ila nikawaza nitakayemwibia atajisikiaje? 

ANGEMNYONYESHA VIPI? 

Anaendeleza simulizi: “Kuhusu kumnyonyesha mtoto ambaye ningemuiba, maziwa ningeyapata kwa gharama yoyote. Kijijini (Mtimblia) kuna dawa unapaka kwenye chuchu za maziwa ya mwanamke.

 “Baada ya muda maziwa yanatoka, yaani ningerudi na mtoto ningejikausha kausha hivyo hivyo kwamba sina maziwa ya kutosha, ningetafuta maziwa ya ng’ombe au kopo, kumbe uzao sio wangu. Ila sikufanikiwa!

 “Ndio maana pale mwanamke anapoiba mtoto kwenye jamii mimpe adhabu kubwa, wengi wao wameathirika na ugumba, naye anajaribu kufidia ile-‘gap’ (pengo) la kukosa mtoto,” anasema. 

 Rai yake ni kwamba wanaothubutu kuiba mtoto, hawastahili adhabu kubwa, akitumia uzoefu wake binafsi na majukumu aliyo nayo sasa, anasema anakuwa ameathirika kisakolojia, huku akilalamika taratibu na sheria ya kurithi au kuasili ina mlolongo mrefu.

 “Jamii ituamini (kinamama) hata sisi ni walezi wazuri, tena tuna upendo ni wachache wenye ukatili ukifuatilia wameathiriwa na tatizo walilokuwa nalo. Nimelea watoto wa ndugu zangu, lakini mwisho wa siku wanarudi kwao,” anasema.

 Shamila anasema wagumba wengi wamekata tamaa, hawana wajukuu kwa sababu hawakuzaa na katika baadhi ya jamii, wanaishia kuitwa wachawi.

 “Sasa nimeamua tu kuikubali hali yangu na kufanya shughuli zingine kwa sababu suala la uzazi limeshanipita, nimehangaika sana hata,” anasema.

 NAFASI YA TIBA

Mwenyekiti huyo wa Chama cha Wagumba, analalamika licha ya kuwapo kliniki za magonjwa mengi, nafasi hiyo kwa wagumba bado haipo.

Anaendelea: “Hospitalini, tiba za uzazi ziko juu. Tuliuliza huduma za upandikizaji hospitali binafsi ilikuwa karibu shilingi milioni 20. Sawa Muhimbili bei imeshuka kidogo, lakini kuna mtu hata shilingi moja hajawahi kuishika.

 “Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya) alitupokea, sasa Jenista Mhagama apokee kilio chetu serikali itusaidie, kwamba sisi tutachangia kiasi kidogo. 

‘Kuna wengine wana ugumba ila hawajapata matibabu sahihi, wakitibiwa watapata watoto...”

 Shamila anaeleza kuona faraja baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzisha kituo maalum cha kuwahudumia, serikali na wadau wengine wa afya, kuwasadia kuchangia gharama za upatikanaji huduma hiyo, takribani Dola za Marekani 5,000 (sawa shilingi 13,611,700), kutokana na wengi wao kuwa na kipato kidogo.

 CHANGAMOTO ZAO

Shamila anasema: “Changamoto zetu nyingi zinafanana, huhitaji wa mtoto. Wengi huduma za afya ya uzazi hawana, pia afya ya akili tatizo wengi wana msongo wa mawazo sababu jamii inatubeza. Kuna wazee ambao hawana watoto nani awatunze, wanashindwa hata mlo mmoja.

 “Kubwa ni kwenye ndoa, tumeshaathirika kisaikolojia utakuta umetoka huku ulikoolewa unasema ukipata mwingine, labda utapata mtoto lakini wapi, utashangaa ndani ya mwaka umepitia ndoa mbili au tatu.

“Unaona kila unayempata hayupo sawa, naye mume anakuona huzai, anakuacha. Mimi niliolewa mara mbili, ndoa ya kwanza nimekaa miaka mitatu na ya pili miaka 11.

“Tangu nilipoachwa mwaka 2006 sijaolewa tena. Nimeamua nikae mwenyewe, ingawa nayo si nzuri, inatakiwa uwe na mwenzako, mimi niliachwa nikiwa na miaka 38 bado kijana.

 “Ni hivi yaani unaweza ukakaa mwaka ‘usishiriki’ na mtu yeyote, unaishia tu kutamani…utakaa na ndugu kweli atakusaidia hata ukiumwa, lakini lazima awepo wa ndani yako, akubembeleze, bora niseme hivi kwa sababu nisiposema ndio magonjwa ya akili yanatujaa.

“Tunaumia na mawazo, sonona unaona dunia haina maana. Kwa hiyo, kuanzishwa hiki chama ni kufarijiana. Hata wizi wa mtoto nilijaribu, mwaka 2006 ili nijinusuru.

“Mume wangu alizaa mtoto wa nje. Kijijini usafiri mwingi ni wa baiskeli. Mwanaume anajali sana yule mwanamke aliyezaa nae, wewe hujazaa huna thamani. Kuna siku (mke mwenzie) alimwita kijana aje amchotee maji, sasa ni lazima atumie baiskeli.

“Mume akasema mpe kijana baiskeli akachote maji, nikamwambia baiskeli yangu haitoki na mimi naenda sokoni. Nikamwambie amkodie baiskeli nitalipia, mume hataki ananiambia nina wivu sababu mwenzangu kapata mtoto, kisa nimezuia baiskeli.

 ‘Nilipigwa sana hadi hupoteza fahamu. Mwisho wa siku nikaachwa. Nikaja mjini Dar es Salaam, niseme nina mimba baada ya miezi tisa nirudi na mtoto, lakini miezi tisa ikatimia sioni pa kuiba.

“Ila nafasi yangu ilinisuta kwa azma hiyo. Ila nami nilitaka niheshimike, maziwa ya kunyonyesha sio shida ningepata maziwa ya ng’ombe na kopo ningenunua na kuna dawa unaweka katika matiti ya mama maziwa yangekuja tu. Hata uongee nini katika familia huna maana,” anaeleza.

Anasema aliwahi kuonyesha nia ya kuwania uenyekiti wa kijiji au udiwani, ila alikwamishwa na hali yake, kwa madai kwamba ‘hana watoto hawezi kuongea...’

 SABABU ZA TATIZO

 Shirika la Afya Duniani (WHO), linataja sababu za ugumba ni kwa mtu yeyote anayeshindwa kushika ujauzito kwa kipindi cha mwaka mmoja, licha ya majaribio mengi kufanya hivyo.

Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka MNH, Dk. Living Colman, anasema: “Mzizi wa 'infertility' inategemea na chanzo, kwa mwanamke chanzo kikuu ni ‘hormonal imbalance' (mayai kushindwa kupevuka kwa mpangilio) na hii inaweza kutokana na ‘genetics’ (nasaba), pia ulaji mbaya, sukari nyingi na mafuta, husababisha unene uliopitiliza.

 “Pia kupungua sana uzito (anorexia nervosa) inaweza kusababisha ugumba. Mirija kuziba ndio sababu ya pili ya ugumba kwa mwanamke na hii husababishwa na ngono zembe kama nilivyoeleza.

Tabibu Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Chama cha Madaktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi (AGOTA), Dk. Julius Kweyamba, anasema tofauti ya kimaumbile ya mji wa mimba kutokuwa ya kawaida kwa mwanamke, ni miongoni mwa sababu wanawake wagumba na wenye utasa.

 “Mama huyu ameumbwa hivyo, mimba zinatoka lakini watu wanakuwa na dhana kwamba huyu hutoa mimba, maumbile hayo ni sababu ya ujauzito kutoka wenyewe.

“Nimeshakutana na baadhi ya kesi (mji wa mimba wenye kasoro) zipo zinazorekebishika na zisizorekebishika,” anasema Dk. Kweyamba.

Bingwa huyo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Francis kilichoko Ifakara, Morogoro, anasema pamoja na ishara kuu na dhana iliyojengwa kwenye jamii kwamba mwanamke anayeona siku zake kila mwezi, uwezekano wa kushika ujauzito ni mkubwa, kutokana na kasoro za kimaumbile.

 Anasema zipo aina sita za mji wa mimba kwa wanawake na kati ya hizo tano huwa na kasoro, ambazo aidha zinaweza kutibika au kutotibika na kuwa miongoni mwa sababu za ugumba kwa mwanamke.

 Bingwa Dk. Living Colman, anaeleza: “Mzizi wa 'infertility' (utasa) inategemea na chanzo. Kwa mwanamke chanzo kikuu ni ‘hormonal imbalance' (mayai kushindwa kupevuka kwa mpangilio) na hii inaweza kutokana na ‘genetics’ (nasaba) lakini pia ulaji mbaya, sukari nyingi na mafuta, husababisha unene uliopitiliza.

 “Pia kupungua sana uzito (anorexia nervosa) inaweza kusababisha ugumba. Mirija kuziba ndio sababu ya pili ya ugumba kwa mwanamke na hii husababishwa na ngono zembe kama nilivyoeleza.

 “Tiba ya ugumba ni kumuona mtaalamu wa afya (gynaecologist) atafanya vipimo na kugundua tatizo halafu atatoa tiba husika. Kama ni ‘hormonal imbalance’ atapewa dawa na ushauri. Kama mirija imeziba atashauriwa apandikize (IVF).

Bingwa wa Afya ya Akili kutoka Idara ya Afya ya Akili, Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH), Dk. Raymond Mgeni, anasema kundi hilo hukumbwa na magonjwa ya akili, kutokana na wengine kunyanyapaliwa.

Makamu Mwenyekiti cha Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili (MEHATA, Bingwa Mwandamizi wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Saidi Kuganda, waliomo kwenye shida hiyo wana maradhi ya msongo wa mawazo na wengine ni sonona.