Ndizo hasi, chanya kuendeleza demokrasia ndani ya miaka 63 ya uhuru

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:39 AM Dec 11 2024

 Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda.
Picha:Mtandao
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda.

TAIFA limeanza safari nyingine ya kuelekea miaka 64 ya uhuru baada ya kumaliza maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru yaliyofanyika juzi, kwa Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.

 Jubilii ya miaka 63 ya uhuru ni ya kujivunia ikiwa na miaka mingi inayovuka nusu karne na kuna mengi ambayo nchi imepitia hadi sasa kukiwa na amani na utulivu baada ya kuwatimua wakoloni waliokuwa wameikalia Tanganyika kabla ya kuwa Tanzania.
 
 Mafanikio mbalimbali yameonekana tangu uhuru, kama ambavyo baadhi ya wadau wa siasa wanavyoyataja, lakini pia matatizo yapo.
 
 Ananilea Nkya ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), anaeleza kuwa nchi inapiga hatua lakini kurudi nyuma au kinyumenyume hasa kwenye kuendeleza demokrasia.
 
 "Tunaendesha siasa ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya nchi, maana  tunapata viongozi  kwa mfumo wa siasa, hivyo tunapofanya uchaguzi unaolalamikiwa kuwa si huru na haki maana yake ni kupata viongozi wanaolalamikiwa pia," anasema Ananilea.
 
 Mwenyekiti huyo anaongeza kuwa  miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi ambao wananchi wanaona kuwa haufuati utaratibu, kanuni na sheria na kwamba matokeo yake wanaochaguliwa kuongoza baadhi si chaguo la wananchi.
 
 "Mfano mmojawapo ni uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni, tumesikia malalamiko na tuhuma zikihusisha baadhi ya taasisi zisizohusika kuingilia uchaguzi badala ya kuusimamia, matokeo yake wananchi na wapigakura wanalalamika.” Anaeleza.


 Anasema utaratibu huo wa uchaguzi unakwamisha maendeleo na kurudi nyuma na kwamba hata enzi ya uchaguzi wakati wa mfumo wa chama kimoja una unafuu kuliko hali ilivyo sasa.
 
 Katika ufafanuzi wake anasema enzi ya chama kimoja, wananchi hawakulazimishwa kuchagua viongozi wasiowataka, walikuwa huru kuchagua mgombea au alama iliyowekwa pembeni ya picha ya mgombea katika karatasi za  kura.
 
 "Hivyo, kwa maoni yangu kuhusu hali ya kisiasa kwa miaka 63 ya uhuru, hatusongi mbele kidemokrasia tunarudi nyuma,” anasema.

Mtaalamu wa uchumi, Steven Machumu.
 
           UTAWALA KISHERIA
 
Mtaalamu wa uchumi, Steven Machumu anasema Tanzania yenye amani na mshikamano, wananchi wake kwa umoja wao wameshiriki kujenga uchumi binafsi na wa taifa bila kubugudhiwa na mtu au mamlaka kwa kuwekewa mazingira wezeshi.
 
Pamoja na hayo, anasema tangu taifa kupata uhuru, limeendelea kusimamia haki za binadamu chini ya katiba kama zilivyoainishwa katika tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu bila kujali itikadi za vyama, dini au jinsia.
 
“Mimi ni mtaalamu wa uchumi, lakini kwa kuwa siasa ni uchumi, nina uwezo wa kuizungumzia. Lakini pia niseme kuwa Tanzania ni mfano kwa amani, upendo na mshikamano Afrika na pengine duniani.”

anasema Machumu.
 
 Anaongeza kuwa hata mifumo huru ya utoaji haki imeendelea kuimarishwa na kuboresha kadri ya mahitaji ya jamii katika kipindi chote cha miaka 63 ya uhuru, kwa kuwa usawa mbele ya sheria umeendelea kuwapo licha ya changamoto za hapa na pale kujitokeza na kurekebishwa.
 
 "Katika kipindi chote hicho, utawala bora wa sheria umeendelea kudumishwa, ukuaji na ujenzi bora wa utawala, sheria na demokrasia vimeendelea kujengwa kwa uangalifu ili kulinda amani ya taifa letu kutokana na uchanga wa demokrasia inayohusisha mfumo wa vyama vingi vya siasa," anasema.
 
 Anafafanua kuwa utawala bora kwa taifa umeendelea kwa kuhusisha taasisi zote za serikali na umma kwa kuhimizwa na kutekelezwa, ingawa  kuna baadhi ya taasisi hujikuta zinapoteza mwelekeo, na kwamba  uwajibikaji umekuwa ukichukuliwa na kurejesha hali ya kawaida.
 
 Vilevile, anasema taifa huru ndani ya miaka 63 limeendelea kuongeza mapambano ya kuzuia na kupambana na rushwa kama adui wa haki kwa wananchi kwa kuunda taasisi maalumu yenye kuhusika na mchakato huo.
 
 Anaongeza kuwa Tanganyika kama taifa lililopata uhuru wake  1961 na kuungana Zanzibar mwaka 1964, muungano huo umeendelea kudumishwa kwa pande zote mbili kwa manufaa ya wananchi wote.
 

Ananilea Nkya ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA).

       MFUMO DUME MWISHO
 
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda, anasema ndani ya miaka 63 ya uhuru, mfumo dume umeendelea kupungua.

Sehemu za kazi, ndani ya vyama vya siasa, uongozi wa kisiasa na kwenye familia kuwapa nafasi za uongozi wanawake kumeonekana, anasema.
 
 Anafafanua kuwa ingawa bado usawa wa kijinsia haujafikiwa kikamilifu, kuna dalili za kuufikia, kwa maelezo kuwa yapo mabadiliko makubwa yanayoendelea kushamiri kuanzia chini hadi juu.
 
 "Mfano, leo tuna rais mwanamke, lakini pamoja na hayo, katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwezi uliopita, wanawake waliogombea nafasi ya mwenyekiti na ujumbe wameshinda," anasema.
 
 Bila kutaja idadi ya wanawake washindi, anasema inatia moyo kuona wanawake wanawania uongozi kwenye ngazi za vitongoji na kushinda, tofauti na miaka ya nyuma.
 
 "Zamani haikuwa rahisi mwanamke kugombea uongozi katika kitongoji au kijiji, kwa sababu ya mambo ya mila na desturi, kwa kuamini kuwa mwanamke hawezi kuongoza, lakini sasa mtindo huo unaendelea kuwekwa kando ndani ya jamii," anasema Mary.
 
 Hata hivyo, anasema pamoja na wanawake kupata nafasi nyingi za uongozi serikalini na katika taasisi za umma, hawapaswi kubweteka, badala yake waendelee kupaza sauti ili kufikia asilimia 50 kwa 50.
 
 "Ni muhimu kufikia asilimia hiyo kati ya wanawake na wanaume, kwa sababu uongozi si kubeba mzigo, bali ni akili na uwezo wa kuongoza, ambavyo wanawake na wanaume wanavyo wote," anasema.