"KASONGO yeye, mombali nagai, Kasongo mbona wewo, songa libala, Kasonge yeye, yeye, Kasongo mbona wewo, mbona wewoo, mombali nanga yeye."
Hiki ni kionjo maarufu zaidi kwenye mitandao ya kijamii , wakati watu wakionesha vibonzo na kutaniana hasa kwenye mambo ya soka.
Haijulikana ni kwa nini kipande hiki kimechaguliwa na watu wengi kuhusishwa kwenye vibonzo, lakini mara ya kwanza kilianza kuonekana kikiimbwa na mchungaji kutoka Uganda, Aloysius Bujingo wa kanisa la 'House of Prayer Ministries' lililopo Makerere kuuimba wimbo huo mbele ya waumini wake.
Kipande cha video ile ambacho alikuwa akiimba, ndicho kimekuwa maarufu zaidi kwenye mitandao ya kijamii, facebook, X, instagram na tik-tok, huwezi kuingia bila kukutana na vibonzo au vichekesho.
Inawezekana kabisa huenda kipande cha wimbo huu kimekuwa maarufu mara baada ya kuchukuliwa na kuingizwa kwenye masuala ya soka.
Pamoja na kwamba kilikuwepo kwenye kichekesho na vibonzo, lakini kilipata umaarufu mkubwa na wa ghafla kilipoingizwa kwenye utani wa soka.
Ilianza Novemba 7 mwaka huu, Yanga ilipofungwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Mara baada ya mechi hiyo iliyokuwa na kipigo cha ajabu, ambapo si mara nyingi kwa timu kubwa kama Simba na Yanga kufungwa idadi kubwa ya mabao, lakini pia ilitoka kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, Novemba Mosi kwenye uwanja huo huo, mashabiki wa Tabora United na wa Simba waliungana kuwananga wale wa Yanga.
Video za kuwananga Yanga ziliambatana na sauti za mchungaji Bujingo iliyokuwa kwenye video aliyokuwa akiimba wimbo huo wa Kasongo.
Kila 'klipu' iliyokuwa inaitania Yanga ilikuwa na kibwagizo hicho, ndipo kilichopata umaarufu mkubwa.
Hata hivyo wengi bado hawajui asili ya wimbo huo, umetoka wapi, umeimbwa na bendi gani na je una maneno yanayofanana na hicho kipande yanayokuwa kwenye utani?
WIMBO KASONGO UMETOKA WAPI?
Huwezi kuuzungumzia wimbo huu kabla ya kuizungumzia bendi yenyewe iliyoupiga. Wimbo 'Kasongo' ulipigwa na bendi ya Super Mazembe iliyoundwa mwaka 1967 nchini Zaire, sasa (DRC) na kuongozwa na Longwa Didos Mutonkole, baadaye ilikwenda nchini Zambia, ambako ilikaa kwa muda na kumpata mwanamuziki,Nashil Pichen, ambaye aliamua kuwachukua na kuamua kuwapeleka jijini Nairobi nchini Kenya na kuweka makazi yake ya kudumu.
Baadaye pia lilibadilisha jina na kujiita, Super Mazembe likiwa na wanamuziki maarufu na nyota kama kina Lovy Longomba, Kasongo wa Kanema, Bukassa Bukalos, Atia Djo, Fataki Lokassa 'Masumbuko wa Dunia', Rondo Kandolo, Charles Atei, Lobe Namapako, and Loboko Pasi na wengine wengi.
Walifyatua nyimbo nyingi zikiwemo 'Kasongo', 'Atia Djo', 'Lovy', 'Gina', 'Loboko', 'Auma', 'Muana Nyau', 'Longwa', 'Samba', 'Lukasi', 'Ouma', 'Okova' 'Mulekeni Marry' na zingine nyingi.
Wimbo wa 'Kasongo' ulifanyuliwa mwaka 1980, ulitungwa na Katele Aley, huku kilichokuwa kiliimbwa ni kikiwa na maana tofauti na vibonzo zinavyoendelea mitandaoni.
"Kasongo yeye, mobali na ngai, Kasongo ngana weo, zonga libala ee..." Haya ni maneno halisi ya kilingala yaliyokuwa akiimbwa kwenye wimbo huo. Ukisoma nakuangalia vizuri hapa utagundua kuna utofauti wa matamshi au mashairi haya na yale pale juu ambapo alikuwa akiimba mchungaji kwani ilionekana hakuyaelewa au kuyatamka vyema maneno ya lugha hiyo maarufu nchini DRC.
Maana yake tafsiri ya kiswahili ya wimbo huo, ni kwamba mwanamke anamsihi mumewe Kasongo arejee nyumbani. "Kasongo mume wangu rudi nyumbani, Kasongo mimi na wewe, rudi nyumbani ee." Ni mke aliyechoshwa upweke, mumewe akiwa ameondoka nyumbani na kumuacha akiteseka na watoto na watoto akiwa hajulikani kama yupo nyumba ndogo au la. Hapo utaona kuwa maana ya wimbo huo, tofauti na hiki kinachoendelea cha kutoana 'akili' na kutaniana kwenye mitandao ya kijamii.
Tuma meseji 0716 350534
Kasongo: Hii ndiyo santuli ya wimbo wa 'Kasongo' ambao kwa sasa umekuwa maarufu sana baada ya zaidi ya miaka 40 sasa. Hapo unajielezea kila kitu, jina la wimbo na mtunzi, Katele Aley.
Mazembe: Hiki ni kikosi cha baadhi ya wanamuziki wa Super Mazembe waliofyatua kibao cha 'Kasongo', mwanzoni mwa miaka ya 1980.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED