MTOTO kuzaliwa na jinsi mbili i ni hali ambayo mtu kuzaliwa na jinsia ya kiume au ya kike. Hapo jinsi zote zinaweza kuwa sehemu moja au sehemu tofauti.
Kimsingi, mwonekano wa nje huwa haueleweki, kwa urahisi kiwango cha mwonekano wa nje wa jinsi hizo hutegemea kwa kiwango cha homoni iitwayo’ tosterone’ inayozalishwa kuanzia wiki ya nane mpaka ya 11 baada ya mimba kutungishwa.
Hivyo, hapo jamii hutakiwa kitaalamu, wasiwafiche watoto hao majumbani na badala yake wafikishwe hospitali, ili waweze kupatiwa matibabu.
Inawezekana jamii haina elimu ya jinsi mbili na hivyo mtoto anapozaliwa huonekana kama ni mkosi na kuamua kumficha.
Ukosefu wa elimu kwa wazazi ni moja ya changamoto inayochangia baadhi ya walezi na wazazi kuwanyima haki zao za msingi watoto wanaozaliwa na jinsi mbili.
Kuzaliwa kwa mtoto kuwa na jinsi mbili, baadhi ya wazazi wanatajwa kuwaficha watoto hao,ili wasiweze kutambulika.
Kutokana na kuwaficha watoto hao, serikali sasa inatoa huduma kwa watoto hao na kuwataka wazazi kutowaficha watoto hao na badala yake, wafikishwe katika vituo vya afya.
Kuwaficha watoto hao ni kuwanyima haki zao za msingi. Hivyo, serikali inawahakikishia wazazi tatizo la jinsia mbili linatibika.
Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema kuwa anatoa wito kwa Watanzania kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye jinsi mbili bali wawapeleke hospitali ili waweze kupata huduma mapema kwa kuwa tatizo hilo linatibika.
Waziri Ummy amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Urolojia Tanzania (TAUS) unaofanyika Jijini Dar Es Salaam.
"Wazazi/Walezi msiwafiche watoto wanaozaliwa na jinsi mbili bali muwapeleke mapema hospitali ili waweze kupata matibabu mapema kwa kuwa tatizo hilo linatibika, lakini pia sio aibu kuzaliwa katika hali hiyo," anasema.
Anasema, mtoto anaweza kufanyiwa upasuaji mapema, akapimwa na akagundulika kuwa yeye ni wa jinsi gani, sio hadi mtoto anakua hajijui yeye ni wa jinsi gani kama ni mwanamke au mwanaume.
Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwa nchi ya kutembelewa kwa ajili ya tiba utalii.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha programu maalumu iitwayo Dkt. Samia Super-Specialized Scholarship Program ya ufadhili wa wataalamu wa ubingwa bobezi ambapo katika mwaka wa Masomo 2023/2024, jumla ya Shilingi bilioni 10.9 zilitengwa kwa ajili ya ufadhili wa wanafunzi 1,109 kwa ajili ya masomo ya ubingwa na ubingwa bobezia," anesema Waziri Ummy.
Anafafanua, kati ya wanafunzi hao 1,109 wanafunzi 33 watakwenda kusomea ubingwa bobezi kwa ongezeko la wanafunzi 26 sawa na asilimia 37 ikilinganishwa na mwaka wa masomo wa 2022/2023 ambapo kulikuwa na wanafunzi 7 wa ubingwa bobezi.
"Kulingana na ufadhili wa programu hii, jumla ya wanafunzi 48 wanasomea udaktari bingwa wa upasuaji urolojia na kati yao madaktari 5 wanasomea ubingwa bobezi wa upasuaji urolojia." anasema.
Kwa upande wake rais wa Chama cha madaktari wa upasuaji Urolojia Tanzania (TAUS) Prof. Sydney Yongolo, anatoa wito kwa madaktari vijana kujiendeleza kimasomo katika fani za ubingwa bobevu kwa kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki katika utendaji kazi ikiwemo kuwatambua madaktari bingwa.
"Tunaendelea kuwasisitiza madaktari kujiendeleza kimasomo hasa kutumia fursa ya programu maalumu iitwayo 'Dk. Samia Super-Specialized Scholarship Program' ya ufadhili wa wataalam wa ubingwa bobezi iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED