SHULE ya Msingi Bokotimiza kwa muda mrefu imeburuza mkia ikishika nafasi ya mwisho kwenye shule za Halamashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Sasa imeondoka kwenye ufaulu wa daraja la C na sasa inaelekea kufikia nafasi ya shule 10 bora za halmashauri hiyo.
Chanzo ni utoro na mwamko mdogo wa wanafunzi, kukosekana ushirikiano wa walimu, wanafunzi na jamii au wanavijiji anasema Mwalimu Mkuu Ridhiwani Mfinanga.
Anaeleza kuwa tangu ahamie katika shule hiyo mwaka 2023 amefanya juhudi nyingi kutengeneza kumaliza utoro uliokuwepo na kuinua ufaulu wa shule hiyo, ambayo sasa inaanza kung’ara.
Anafafanua:“Niliwafuatilia wanafunzi vinara wa utoro na kuzungumza nao kuelezana sababu ili niweze kutafuta ufumbuzi kwa kutumia vyanzo halisi.”
Anasema amewarejesha wanafunzi 10 wa darasa la saba shuleni ambao hata hivyo katika mtihani wa taifa hawakufanya vizuri japo wamepata vyeti vya kuhitimu mwaka 2023.
Mwalimu huyo anasema mwaka 2023 waliohitimu elimu ya msingi Bokotimiza walikuwa 79 kati yao 69 walifaulu, mwaka 2024 wanafunzi 94 walihitimu 86 walifaulu na ni kipindi ambacho shule hiyo iliondoka kwenye kundi la kuwa wa mwisho ngazi ya halmashauri na sasa ni miongoni mwa vinara ikielekea kufika 10 bora.
“Tulianza kuondoka kwenye nafasi ya mwisho pamoja na kuendelea kuwa na ufaulu wa wastani wa daraja C ukilinganisha na ilivyokuwa awali.”
Anasema ufaulu huo ni matokeo ya juhudi za kudhibiti utoro na pia kuongeza ushirikiano baina yao na wazazi,walezi na jamii.
“Awali wazazi na walezi wakiitwa hapa shuleni walikuja kwa shari kama vile walimu ni adui zao hali hii tumeibadilisha na sasa wananchi, wazazi wa wanafunzi na walimu tumeimarisha ushirikiano kila jambo tunajadili kwa pamoja na kulitafutia utatuzi,” anasema Mfinanga.
Mbali na hayo anaeleza kwamba kushuka kwa ufaulu kulichangiwa na njaa na hivyo wameanzisha utaratibu wa chakula ambacho wanafunzi wanachangia Sh. 500 kila siku ili wapate chakula jambo ambalo wameafikiana na wazazi na linaendelea kutekelezeka.
“Njaa ilikuwa inashusha ufaulu kwakuwa wanafunzi wanaingia asubuhi hadi mchana hawajala chochote. Ukifundisha wakiwa na njaa hawakuelewi. Tumeanzisha utaratibu wa chakula na sasa tunashuhudia mabadiliko. Shule nyingine naomba ziige tunachofanya,” anasema Mfinanga.
Sambamba na yaliyofanyika katika kuinua ufaulu na kudhibiti utoro, Mfinanga anaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ukarabati wa vyumba vya madarasa vilivyokuwa vimechakaa.
Shule hiyo ina wanafunzi 735 tayari 698 wameripoti tofauti na miaka mingine ambapo kipindi kama hicho asilimia kubwa walikuwa bado nyumbani.
Shule hiyo pia ina uhitaji wa madawati 56 kati ya 266 yanayohitajika, nyumba sita za walimu zilizopo ni nne, vyumba vya madarasa ni saba kati ya 11 vinavyohitajika pamoja na matundu ya vyoo 18 ukilinganisha na yaliyopo sita kati ya 24 yanayohitajika.
Mmoja wa walimu wa shule hiyo Felista Msemwa, anasema awali wazazi walikuwa hawana mwamko wa kuwahamasisha wanafunzi kwenda shule zinapofunguliwa tofauti na sasa.
Anasema utoro wa mwaka 2023 na miaka mingine ya nyuma ulikuwa mkubwa tofauti na sasa na pia wanafunzi waliokuwa wanaripoti kwa wakati wakiwa na vifaa vyote vinavyotakiwa yakiwamo madaftari.
“Wazazi na walezi wengi walikuwa hawawahishi wala kuhimiza watoto wao umuhimu wa shule. Walijenga dhana kwamba siku za mwanzo ni za kufanya usafi na hakuna ratiba za masomo, inaweza ikatokea mfano kati ya wanafunzi 700 siku ya kwanza wanaweza wakaripoti100 pekee tofauti na mwaka huu ambapo siku ya kwanza walifika 600 kati ya 735,” anaeleza Felista.
Aidha, anasema mbali ya mwamko huo wa wanafunzi kuripoti shule kwa wakati pia wanafika wakiwa na vifaa vyote vinavyotakiwa ikiwemo daftari na kalamu jambo ambalo ni mabadiliko makubwa yaliyofanyika kutokana na kuimarisha ushirikiano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule Ramadhani Mkweche, anaeleza kwamba kamati yao katika kuboresha miundombinu imeanza na kukarabati miundombinu ya maji shuleni na kuunganisha umeme.
Mkweche anasema wamekubaliana na wazazi kuendelea kushirikiana kwa michango mbalimbali kujenga maboma ya vyumba vya madarasa ili serikali iweze kuyamalizia na kupunguza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa.’’anasema.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo Najma Bakari pamoja na Dickson Christopher, wanasoma darasa la saba wanashukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya madarasa pamoja na madawati.
Ajuaye Mohamed mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo anaeleza kwamba mabadiliko yaliyofanyika yataongeza ufaulu kwa wanafunzi shuleni.
Ajuaye anasema awali wanafunzi ikifika saa nne asubuhi walionekana mitaani wakizurura bila sababu na wengine hawakwenda shule jambo lililochangia kupata matokeo mabovu.
Kwa upande wake Omari Mpoto, ambaye pia ni mkazi wa Bokotimiza anasema ufaulu umeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma hali hiyo imechangiwa na ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walezi na walimu.
Pia anasema uelewa wa umuhimu wa elimu kwa watoto umekua na kuongezeka hivyo wazazi wengi sasa wanawafuatilia na kutafuta mafanikio na maendeleo ya watoto wao.
Katika shule hiyo matokeo mabaya yanaelezwa kwamba yalipatikana mwaka 2019, 2020 na mingine ya nyuma lakini kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2022 hali imeanza kubadilika kwa kuondoka kwenye matokeo ya shule 10 duni za halmashauri hiyo.
Pamoja na kuanza kwa ujenzi wa maboma ya vyumba vya madarasa wananchi wanaomba kuungwa mkono na wadau wa ndani na nje ya kata hiyo kuyakamilisha na kuondoa msongamano wa watoto darasani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED