Ziara ya Samia Korea yavuna trilioni 6.481/-

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 09:16 AM Jun 03 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol, kabla ya kushuhudia hafla ya utiaji saini mikataba mbalimbali baina ya nchi hizo iliyofanyika Ikulu Seoul jana.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol, kabla ya kushuhudia hafla ya utiaji saini mikataba mbalimbali baina ya nchi hizo iliyofanyika Ikulu Seoul jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Korea, Yoon Suk Yeol, wameshuhudia utiaji saini wa mkataba mmoja, Hati za Makubaliano (MoU) mbili na tamko la pamoja la kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA).

Tukio hilo lilifanyika jana katika Ikulu ya Jamhuri ya Korea katika Jiji la Seoul, wakati wa ziara rasmi ya Rais Samia kwa mwaliko wa kiongozi huyo, ikiwa ni ya pili kufanyika kwa miaka 26 baada ya Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, mwaka 1998.

Aidha, manufaa ya moja kwa moja kwa Tanzania baada ya kutia saini kwa nyaraka hizo ni mkataba wa kuiwezesha nchi kupokea mkopo kutoka Korea wa Dola za Marekani bilioni 2.5 kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2028.

"Fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF). Ili kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, Tanzania na Korea zimesaini pia mkataba wa EPA utakaowezesha kuufanya uhusiano kuwa wa kimkakati hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji, viwanda na usafirishaji," ilifafanua taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Makubaliano hayo yana lengo la kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa Mkataba wa Ushirikiano wa kiuchumi na Korea, na kwamba nchi zingine ni Morocco na Kenya.

Hati za makubaliano zilizotiwa saini leo ni pamoja na Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu ambapo Tanzania itashirikiana na Korea Kusini katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na utafiti wa masuala ya bahari, kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania kupata ajira za moja kwa moja na nyinginezo ikiwamo ukuaji wa uchumi.

Pia Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Korea Kusini zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Madini ya Kimkakati.

"Tanzania na Korea Kusini zitashirikiana katika utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati nchini Tanzania. Madini hayo ni Nickel, Lithium na Kinywe," ilifafanua taarifa hiyo.

 Aidha, Rais Samia amependekeza ushirikiano wa sekta nyingine mpya zikiwamo maendeleo ya nishati ya gesi asilia, sekta ya ubunifu ya sanaa na filamu; na kufunguliwa kwa soko la ajira la nchini Korea kwa vijana wa Tanzania kupitia mpango wa 'Employment Permit System' (EPS).

Ziara ya Rais Samia ni ya kimkakati kutokana na fursa nyingi zilizopo kwa Tanzania kwenye maeneo ya biashara, madini, miundombinu na mazao kwa kipindi ambacho Korea inajitanua kufungua milango kwenda Afrika na kwamba biashara kati ya nchi hiyo na dunia, Afrika inaambulia asilimia moja pekee.

Nchi hiyo ambayo ni ya 13 kwa uchumi mkubwa dunia inafungua masoko mapya kutokana na somo walilolipata wakati wa COVID-19 wakitegemea nchi za China, Japani na Urusi kupata malighafi, lakini walifunga hali iliyosababisha upatikanaji wake kuchukua muda mrefu.

Aidha, kutokana na hali hiyo walitafuta mbadala wa mnyororo wa usambazaji, huku sababu nyingine ni kufikia lengo la dunia la kuondoa hewa ukawa kwa asilimia 50 wakitaka kutumia nishati jadidifu, lakini wanakosa malighafi za betri na ndio sababu ya kuifikiria Afrika.

Pia sababu nyingine ni soko la Korea kubwa kuwa Ulaya na Marekani ambako kuna sheria kwamba ili kampuni za nchi hizo (Marekani na Ulaya) zizalishe bidhaa bila malighafi kutoka China, ndio sababu ya kutafuta uhusiano na nchi za Afrika ili kutafuta fursa.

KWANINI TANZANIA

Tanzania imetokea kupendwa na Korea ikiwa ni miongoni mwa nchi saba za Rwanda, Ghana, Msumbiji, Senegali, Ethiopia na Uganda.

Inaongoza kupata misaada na mikopo ya miradi nafuu baada ya Misri inayopata jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.6 na Tanzania ikifuata kwa Dola bilioni 1.3.

Tangu kuanza uhusiano wa Tanzania na Korea mwaka 1992, kwa miaka mitano misaada iliyopokelewa mwaka 2014-2020 zilitolewa dola milioni 733 ambazo zilitumika kwenye mradi ya ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Mlonganzila Muhimbili, Daraja la Maragarasi, Mradi wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mradi wa umwagiliaji Zanzibar.

Aidha, mwaka 2021-2025 serikali ilisaini miradi ya Dola bilioni moja, ambayo ni upimaji ardhi kwa dijitali  utawekeza data za viwanja kidijitali, Chuo cha Tekonolojia Kijiditali (DTI), Ujenzi wa Hospitali ya Miguni Zanzibar ya vitanda 600.

Pia kuna mradi wa Dola milioni 230 wa kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambayo itakuwa ni maghorofa na kwamba ujenzi utaendelea huku huduma zikiendelea na hadi 2030 utakuwa umekamilika.

Miradi mingine ni Visiwani Zanzibar kitajengwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano, Bandari ya Uvuvi Bagamoyo na Chuo cha Reli cha Kisasa, na kwaamba nyongeza ya mkopo wa Dola za Marekani bilioni 2.5.

Kutokana na mikopo hiyo Tanzania itaamua miradi ya kutekeleza na riba yake ni asilimia 0.001 utakaolipwa kwa miaka 40 na inalipwa baada ya miaka 25.

Nguvu kubwa itaelekezwa kwenye ushirikiano katika madini ya kimkakati na kwamba Tanzania imedhamiria kuweka nguvu eneo hilo kwa kupima kwa kuwa asilimia 16 pekee ndio yamepimwa kwa kuwa wana teknolojia kubwa.

Katika eneo la madini Tanzania imejipanga kimkakati kwa kuongeza thamani ya madini ili kuhakikisha wananchi wananufaika.

Eneo jingine ni kufungua uchumi wa bahari (uchumi wa blue) na kwamba Rais Samia na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ambako Tanzania haijavuna kwa kuwa kuna samaki aina ya Jodari ambao wana soko kubwa duniani kutokana na malighafi inayopatikana.

Aidha, nchi hiyo ina mikataba ya biashara 21 na nchi 28 duniani na tamko hilo linalenga la kuanza mazungumzo ya kuingia mkataba ambao ndani yake una fursa nyingi kwa Watanzania ikiwamo bidhaa za nchi kwenda moja kwa moja Korea.

Rais Samia amehitimisha ziara rasmi ya siku mbili na anatarajia kuanza ziara ya kikazi kwa kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika, ambako atatoa maoni katika jopo la Kuimarisha Usalama na Chakula na Madini.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema kiongozi huyo kupata nafasi kutoa maoni yake kwenye mkutano huo ni jambo kubwa linalotokana na kazi nzuri iliyofanyika kwenye mtandao wa barabara na kuunganisha reli unaoifanya Tanzania kuwa bora zaidi.

Katika ziara hiyo, Rais Samia anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causal) na Chuo Kikuu cha Anga Korea (KAU) kwa kutambua mchango wake katika mabadiliko ya sera na uongozi wa kimantiki.

Tayari kiongozi huyo ana shahada tano za heshima baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharial Nehru cha India na Chuo Kikuu cha Ankara, Uturuki, wote wakitambua mchango wake kwenye nyanja mbalimbali.