Watu 30 kufanyiwa upasuaji wa nyonga, magoti wengi shida uzito

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 04:38 PM Feb 14 2025
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko
Picha: Christina Mwakangale
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, inatarajia kuwafanyia upasuaji wa marejeo wa upandikizaji wa nyonga na magoti, kwa watu takribani 30, huku wenye tatizo wengi ni wanene na wanawake.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko, ameyasema hayo leo, Dar es Salaam, kwamba upasuaji huo utafanyika katika kambi maalum kuanzia Februari 26 hadi Machi 7, mwaka huu.

Amesema tangu kuanza kwa huduma ya Upandikizaji nyonga na magoti, mwaka 2023 waliokwishahudumiwa ni 263 baadhi yao chanzo likiwa ajali, umri, jinsi hasa wanene kupindukia.

“Hospitali imeendelea kujikita katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi na katika kuhakikisha huduma hizi zinakuwa endelevu na kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya afya tumeandaa kambi maalum.

“Upasuaji wa marejeo (revision) wa kupandikiza nyonga na magoti, utafanyika kwa kushirikiana na Bingwa Mbobezi wa Upandikizaji wa Viungo kutoka China, Dk. Tian Hua, ambaye amebobea katika eneo hilo,” alisema Dk. Mfuko.

“Kufanyika kwa kambi hii kunatokana uhitaji wa watu wengi wanaokuja kutafuta huduma hiyo hospitalini hapa na kutofanikiwa. Uongozi ukaona ipo haja ya kuwapunguzia usumbufu wa maumivu na gharama za kutafuta huduma hizi nje ya nchi,” amesema.

Bingwa wa Nyonga na Magoti kutoka MNH-Mloganzila, Dk. Abubakar Hamis, amesema kutokana na waliofanyiwa huduma hiyo kufanyika wakati teknolojia ikiwa duni, ndio sababu kuu ya kufanyiwa upasuaji wa marejeo.