Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameendelea na jitihada za kuhamasisha wakulima kulima kilimo cha kisasa cha pamba ili kuongeza mavuno na kuinua uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.
Akiwa shambani leo Februari 19, 2025, katika wilaya ya Shinyanga, RC Macha alisema kuwa ziara yake ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyemtaka kurudisha heshima ya zao la pamba mkoani humo.
Kipindi anaapishwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,moja ya maelekezo ambayo alipewa ni kurudisha heshima ya zao la pamba mkoani humo.
RC Macha amesema huo ni mwendelezo wa ziara zake, kwa kutembelea wakulima shambani na kuwahamasisha kufanya kilimo cha kisasa, sababu pamba ni zao kubwa la kiuchumi mkoani Shinyanga, maarufu kama dhahabu nyeupe.
"Lengo la ziara yangu kutembelea mashamba ya pamba, ni kutekeleza agizo la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, la kurudisha heshima ya zao la pamba hapa mkoani Shinyanga,na kuinua uchumi wa mkulima na Taifa kwa ujumla,"amesema RC Macha.
Amesema wakulima wa pamba mkoani Shinyanga,kipindi cha nyuma walilegalega kulima zao hilo sababu ya kulima kiholela na kupata mavuno kidogo na kushindwa kuinuka kiuchumi,na kwamba yeye akiwa ameambatana na wataalamu kilimo, ameamua kuingia shambani ili kuhamasisha kilimo cha kisasa.
"Nilipofika hapa Shinyanga nilikuta hekali moja ya pamba mkulima anapata kilo 250 hadi 300, lakini sasa hivi nahamasisha walime kisasa ili wapate kilo 1,200 kwa hekali moja na kuendelea,mavuno ambayo yatawakwamua kiuchumi," amesema Rc Macha.
Amesema kwamba, historia ya zao la pamba mkoani humo inaonyesha wapo wakulima ambao walishawahi kupata kilo 1,800 hadi 2,000 kwa hekali moja na zaidi,na kueleza kwamba kilimo cha kisasa ndiyo mkombozi mkubwa wa mkulima.
Aidha, amesema katika ziara yake hiyo ambayo amezunguka mkoa mzima, kwamba ameridhika na wakulima wa pamba kwa kufuata kilimo cha kisasa, sababu amejionea mwenyewe kwa vitendo maendeleo ya zao hilo shambani.
Amevitaka pia Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), kwamba kipindi cha kununua pamba ya mkulima, wainunue kwa uaminifu na kwa vipimo sahihi ili kutompunja mkulima.
Amewataka pia wakulima wa pamba, kwamba wanapovuna pamba yao na kwenda kuiuza wasiichafue, kwa kuweka maji na mchanga.
Nao baadhi ya wakulima wa pamba akiwamo Andrew Maganga kutoka Kijiji cha Sayu wilayani Shinyanga, amesema yeye amekuwa akilima kisasa kwa kupanda mbegu za pamba sentimita 60 kwa 30, na amekuwa akipata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.
Amesema mwaka jana alilima pamba hekali moja na robo ambapo alipata Kilo 2,760, na alikuwa mshindi wa pili kitaifa kwa uzalishaji wa pamba, na alipewa zawadi ya sh.milioni 5 na Serikali.
Naye Mkulima George Bulugu,amesema yeye mwaka jana alilima hekali 2 za pamba kisasa, na alipata kilo 1,800 na kwamba mwaka huu anatarajia kupata mavumo mengi zaidi.
Mkulima Shimba Sprian, ametoa wito kwa wakulima wa pamba,kwamba wazingatie ushauri ambao wanapewa na wataalamu, kwa kufanya kilimo cha kisasa tangu maandalizi ya shamba,ili wapate mavuno mengi kama wao wanavyofanya na kujikwamua kiuchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED