KINAMAMA wako kwenye kampeni ya kupiga debe, wanaume wawasindikize wake zao kliniki, ikiwa njia ya kujenga upendo wakati wote wa ujuzito na baada ya kujifungua.
Hatua hiyo, pia inatajwa kuwasaidia kujenga furaha kwa mjamzito, pia ikimfanya mwanaume kujua mengi yanayohusu afya ya uzazi, zao lake ni uwezekano wa mjamzito kujifungua mtoto mwenye afya njema.
Pamoja na kampeni hiyo kudumu muda mrefu, inaelezwa kuwa mwitikio wa wanaume kuwasindikiza wake zao kliniki bado ni mdogo na inatokana na sababu mbalimbali zinazoelezwa na mdau wake kuwa ‘hazina mashiko.’
Mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Agness Mgaya, anasema kuna mwitikio mdogo wa wito kwa wanaume kuambatana na wake zao kliniki au safari ya kwenda kujifungua.
Hapo anataja takwimu za mkoani kwake katika mafunzo ya huduma za dharura kwa wakunga wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya za mkoa na za rufani mkoani humo, yaliyofanyika wiki hii.
"Kuna idadi ndogo ya wanaume ambao wanaongozana na wake kwenda kliniki ni kama asilimia 40 tu! Wengine hawaendi wakiwa na sababu ambazo hazina mashiko," Mratibu Agness, anaeleza. Anasema kuwa, mwanaume anapoambatana na mke kwenda kliniki au kujifungua, anafundishwa mambo mengi ya kumsaidia kutoa huduma za awali kabla ya kumfikisha katika kituo cha afya.
"Ikumbukwe, mjamzito anaweza kuumwa kichwa zikiwa ni dalili za kifafa cha uzazi, lakini mume akampa panadol akadhani ni maumivu ya kawaida, hapo atakuwa hajatatua tatizo," anasema.
Anaongeza kuwa, mume anapoambatana na mkewe kliniki, anafundishwa mengi ya msaaada kuhusiana na huduma za awali kabla ya kumfikisha mama katika kituo cha afya na njia hiyo inasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Kwa mujibu wa Mratibu Agness, mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa una vituo 35 vinavyotoa huduma ya upasuaji na kufafanua kuwa, kuna wastabni wa wawanawake 157,000 wanaojiofungua kila mwaka.
SABABU ZA KUKWEPA
Agness anataja baadhi ya sababu zinazochangia kuwapo mwitikio mdogo wa wanaume kuwasindikiza wenza wao kliniki, ni pamoja na kuelemewa na majukumu ya kila siku. Hata hivyo, anakinzana na hoja hiyo, akifafanua kwamba ni hali inayotatulika, iwapo kila mwanaume atatambua umuhimu wa kuhudhuria kliniki na mwenza wake, atanue uelewea wake kuhusdi jambo hilo.
"Wataalam wa afya wanasisitiza umuhimu wa mama kuhudhuria kliniki na mwenzake, ili kupatiwa ushauri wa namna ya kulea ujauzito, lakini baadhi ya wanaume jijini Dar es Salaam wanakwepa," anasema. Mratibu huyo anasema, suala la mume kumsindikiza mke wake, halishii wakati wa ujauzito tu, bali pia hata baada ya mzazi wakati wakiwa tayari wamejifungua ili wapate elimu ya afya ya uzazi na umuhimu wa kunyonyesha watoto.
"Mwanaume yeyote anayejali mwenzi wake na ujauzito wake ana wajibu wa kumsindikiza kliniki mahudurio yote nane, kabla na baada ya kujifungua kuonyesha upendo na ushirikiano kati yao," anasema.
MAFUNZO KWA WAKUNGA
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dk. Beatrice Mwilike, anasema kuna umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo kwa wakunga nchini, ili kujiongezea ujuzi wa kazi yao.
Dk. Beatrice anasema, kumekuwapo changamoto nyingi katika masuala ya uzazi, zikitokana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba, wakunga wanapaswa kujua namna ya kukabiliana nazo.
"Wakati mwingine mjamzito anaweza kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua au kushindwa kujifungua, hivyo ni muhimu mkunga awe na mbinu za kusaidia kumaliza tatizo," anasema Dk. Beatrice.
Anasema, wapo watoto wanaopoteza maisha siku chache baada ya kuzaliwa, na kwamba kupitia mafunzo mbalimbali yanatolewa kwa wakunga, wanaweza kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 90.
"Mafunzo kazini yana umuhimu mkubwa wa kumsaidia mkunga kufanya kazi yake kwa usahihi zaidi, kwani anakuwa na uwezo wa kufanikisha utoaji wa huduma bora, ambazo zitakuwa na mchango mkubwa wa kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga," anasema.
Rais huyo anasema, mafunzo hayo ni sehemu mradi wa miaka saba uitwao 'Thamini Uzazi Salama' uliozinduliwa Dar es Salaam mwaka jana, ukihusisha pia, mkoa wa Shinyanga.
"TAMA inashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Tanzania na Chama cha Wakunga cha Canada kuendesha mradi huu na tunatarajia kufikia wakunga 600," anasema. HALI YA VIFO
Miaka minne iliyopita, inatajwa vifo vilivyotokea wakati wa kujifungua vilikuwa 556 kati ya wajawazito 100,000 waliofika hospitalini kupata huduma ya uzazi, sasa vimepungua kutokana mabadiliko ya huduma za afya yanayoimarishwa.
Moja ya mabadiliko, ni uwekezaji mkubwa katika afya kwenye majengo mengi, upatikanaji vifaa tiba na kusomesha wafanyakazi, hatua iliyopunguza vifo vya wajawazito kutoka 556 mpaka 104.
Hatua hiyo ya kupunguza vifo, imemfanya Rais Samia Suluhu Hassan, kupata tuzo iliyotolewa na taasisi ya The Gates Foundation, kwa kutambua mchango wake katika kuboresha afya nchini. Wakati akipokea tuzo hiyo, Rais akasema malengo ya dunia ifikapo mwaka 2030 kufikiwe wastani wa vifo 70, kati ya 1,000, akiamini nchi itafika huko au kuvuka malengo hayo ya dunia.
Anasema serikali imeongeza idadi ya madaktari bingwa waliosajiliwa kutoka 69 mwaka 2020 hadi 338 mwaka 2024, na kumewapo huduma za afya za uzazi bila malipo na kwa watoto chini ya miaka mitano. Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia. Serikali imeimarisha mifumo ya rufani kwa kuongeza magari 727 ya wagonjwa katika kipindi cha miaka tisa, kuanzia 2015 hadi mwaka jana.
Pia, inatajwa kuimarishwa upatikanaji huduma za dharura za uzazi, kwa kuziba pengo kati ya jamii za vijijini na vituo vya afya. Rais Samia anasema serikali pia imeanzisha huduma za rufani za dharura za mama na mtoto aliyezaliwa na kuongeza idadi ya mashine za ‘ultrasound’ kutoka 345 mwaka 2020 hadi 970 mwaka 2024.
Hatua hiyo pia imeenda sambamba na uboreshaji barabara za vijijini, pia kuanzishwa programu itwayo M-MAMA, inayohakikisha wajawazito wanapata usafiri wa dharura hadi kwenye vituo vya afya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED