KATIKA maisha ya kila siku, miongoni mwa yaliyoiteka jamii duniani, imo upenzi au ushabiki wa soka.
Hali hiyo ya ushabiki, inatafsiriwa kitaalamu kwenye stadi za lugha kuwa “tabia au hali ya kupenda sana au kupapatikia jambo au kitu...”
Pia, yatokanayo na ushabiki huo sasa mahsusi kwa vilabu vikongwe nchini, Simba na Yanga unazaa jipya linaloendana nalo, kiulizo cha afya ya akili katika yale yanayotendwa na mashabiki wake.
Wataaluma wa afya nchini nao wanatafsiri “afya ya akili ni jinsi tunavyoishi, uamuzi tunayochukua, jinsi tunavyoona, mawazo yanayokuja.
“Ni kwa sababu ya kile kilicho akilini. Ikiwa mtu anataka kutembelea bustani, anaitembelea kiakili kwanza na kisha kimwili....”
Ikirejewa maudhui sita kati ya 15 ya wasifu wa shida katika afya ya akili kitaalamu, yanaendana na baadhi ya yanayoshuhudiwa sasa kutoka ushabiki wa soka nchini, mahsusi vilabu vikongwe; Simba na Yanga, vyenye umri unaosonga karne sasa.
Baadhi yake ni matendo yenye viashiria vya mabadiliko ya akili na kisaikoliojia, kama vile wasiwasi, matatizo binafsi yanayoigusa hisia na ustawi wa kijamii uanoathiiri hisia, fikira na maisha ya watu kila siku.
Pia, inatajwa kuwa hali inayoendana na: Kupunguza uwezo wa kuzingatia; kujiondoa kutoka miunganisho ya kijamii na shughuli za kila siku kimaisha; kujitenga na ukweli kwa kuegemea dhana potofu; kushindwa kuelewa hali na watu; vilevile hasira, uadui na vurugu
KINACHOJIRI ULINGONI
Mvutano wa kiushabiki wa soka, kati ya wapenzi wa Yanga na Simba inaonyesha ishara za mmomonyoko wa maadili, yakiwa dhahiri katika maeneo tofauti ya kijamii.
Viashiria vya wazi vina ushuhuda katika matumizi ya lugha chafu kwa umma, zinazogeuka kero kwa umma unaolazimishwa kuzisikiliza, hali hiyo ikizidi kusambaa katika maeneo na matukio mengi.
Sehemu mojawapo ni kwenye vituo vya mabasi dalaladala, bajaji na bodaboda, katika migahawa ya vyakula na vinywaji, imekuwa mithiili ya kawaida kusikia mtu akitaja ‘faragha’ ya mtu kwa uhuru, zaidi wakishambuliwa kinamama kwa nafasi tofautii.
Mfano hai, ni tukio la aliyejitambulisha yu shabiki timu mojawapo kubwa, akitambulisha kwa jina la umaarufu wake ‘Shetani wa ...Yanga’, aliyerekodiwa kwenye mtandao wa kijamii.
Huyo akaahidi kumuweka rehani mama yake abakwe, iwapo klabu mpinzani wao angeifunga timu nyingine (anaitaja) inayocheza nayo ligi moja, huku akitumia kauli lugha ya kabila mojawapo kupunguza makali ya kauli yake.
Hapo ndio ugumu na uhalalali kisaikolojia unachukua nafasi, ingawa timu hizo za soko hazijichagulii mashabiki, bali zinawakuta.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa viongozi wenye maadili wanaweza kuweka mkakati wa kuhakikisha wanakuwa na mashabiki wanaozingatia maadili, pia kulinda heshima za hizo timu.
Shabiki huyo baadaye akaonekana kajitokeza tena kuomba msamaha kwa kilio ‘kujutia’ alichotenda, ingawaje kuna watu mashuhuda waliohoji ‘kama kilikuwa kilio cha kweli...” huku ikidaiwa hata klabu husika haikukubaliana naye.
Hapo akawashukuru wanahabari, akijinadi upande wa pili sasa ni maarufu kuzidi msanii mmoja anayemtaja jina nchini.
Hiyo, inawarejesha hata wanahabari kutathmini upya, majukumu yao kitaaluma na usalama kimaadili, ikibeba viasharia vya afya ya akili, kuhusiana na uhamasishaji vitendo vya kikatili kama hicho, kunadi dhana ya mama yake kubakwa.
Inatajwa kuwa kiashiria kigumu chenye maswali, huku kukiwapo matumizi ya misamiati kama ‘shetani’ katika ustawi wa kiimani katika jamii, vinginevyo inaacha utata wa kisaikolojia kuoanisha matumizi yake.
Sifa za vitendo vya ‘ushetani’ inavyotambulika kwa njia zote; lugha, kijamii na matendo ya Imani kwamba ni dhana za kukosekana uadilifu, pia uovu.
Ndio inaongeza uhalali wa kifikra na kimamlaka, shabiki kupata ujasiri wa kutamka na kuitenda hadharani hayo.
Kuna dhana zinazotanda zikiambatana na hizo zikidhalilisha nafsi binafsi, pia wenza wao katika ushabiki wa soka ndani na nje ya nchi.
Kimaadili, inatajwa ni kawaida kushuhudiwa mume anayejitambua anampa thamani mkewe, staha za usalama wa afya ya akili.
Ni sababu zinazofikisha dhana hizo katika elimu za umma rasmi na zisizo rasmi, pia katika nguzo za imani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED