Watiania CHADEMA walia usaili unatisha

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:55 AM May 14 2024
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA wakiwa katika kikao cha kusaili wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho Dar es Salaam jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Benston Kigaila, Katibu Mkuu, John Mnyika, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu.
Picha: Elizabeth Zaya
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA wakiwa katika kikao cha kusaili wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho Dar es Salaam jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Benston Kigaila, Katibu Mkuu, John Mnyika, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu.

WATIANIA ya kugombea nafasi za uongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesema usaili wa chama hicho si wa masihara.

Baadhi wamedai kuulizwa maswali magumu, wakiyaita ya "uchokonozi", wakisisitiza maswali yalikuwa mengi zaidi kwa watiania ambao walishawahi kushika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.

Usaili wa watiania jana ulianza sita mchana. Hata hivyo, hadi saa 10 jioni ni Kanda moja tu ya Magharibi ambayo ilikuwa imefanyiwa usaili.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wajumbe wakitoka ukumbini kwa ajili ya mapumziko ya chakula saa 10:15 jioni.

Baadhi ya wagombea ambao waliofanyiwa usaili walisema maswali wanayoulizwa ndani na wajumbe wa kikao hicho ni magumu.

"Ndugu yangu, huko ndani ni kwa moto, mambo yanayoulizwa ni mengi, wanakuchokonoa kila kitu na vile vichwa vilivyokaa kwenye usaili viko moto, vina madini mengi," alisema mmoja wa watiania.

Alidai kuwa miongoni mwa vitu alivyoulizwa ni namna alivyokitumikia chama, pia mipango na mikakati yake kukiletea ushindi katika uchaguzi zijazo.

"Pia kulikuwa na maswali ya uchokonozi kuhusu mienendo ya kitabia na kama niliwahi kutuhumiwa kwa makosa yoyote," alisema huku baadhi ya wagombea wakilazimika kutoka eneo la ofisi ya chama hicho kwenda kutembea, wakidai "kuvuta muda".

Akizungumzia muda uliotumika kuhoji watiania hao, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, alisema mahojiano kwa mtu aliyewahi kugombea au kuwa kiongozi na ambaye ni mpya hayafanani.

"Yule aliyewahi kugombea ni lazima awe na mambo mengi ya kuhojiwa, alikifanyia nini chama, alifanikiwa au alishindwa wapi na kama alishindwa ni kwanini na mengine mengi, ni tofauti na anayeanza," alisema Mrema.

Mtiania ya Uenyekiti Kanda ya Magharibi ambaye anatetea nafasi yake, Gaston Garubindi, alisema alitumia nusu saa kufanyiwa usaili.

"Mimi kwa sababu ni kiongozi, nimehojiwa vitu vingi na lazima watake kujua nimekifanyia nini chama na huko ninakotaka kwenda," alisema Garumbindi.

Alibainisha kuwa jumla ya viongozi na wajumbe walioshiriki katika usaili huo ni  zaidi ya 30.

SUGU ALONGA

Mtiania ya Uenyekiti Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, alipoulizwa kama ana uhakika kwa kuteuliwa na kamati kuu kugombea nafasi hiyo, alisema hana shaka na hilo.

"Nimejipima ndio maana nikaamua kugombea, kama ningeona kuna wingu nisingegombea, hivyo nimejiridhisha nimeamini kwamba nitapita usaili na nitapita kwenye uchaguzi.

"Kwanza kutoteuliwa ni lazima uwe na upungufu, mimi nimejipima na sina upungufu ambao utafanya nisiteuliwe na ninaamini kwamba kamati iliyopo humo ndani ina nia nzuri na wameweka mchakato wa kidemokrasia ili ipate wagombea bora ambao chama kinawataka," alisema Sugu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho, usaili unatarajiwa kukamilika leo.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho kabla ya kuanza kwa kikao hicho, mada zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa ni tatu, ikiwamo kupokea taarifa ya uchaguzi, kupokea tathmini ya maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa na kuweka mwelekeo wa awamu ya pili ya maandamano.

Nyingine ilikuwa kufanya usaili wa kuteua wagombea nafasi za uongozi katika Kanda Nne za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi.

Kwa mujibu wa Mrema, usaili wa wagombea ulitakiwa kumalizika juzi ukishirikisha wagombea wa nafasi za Uenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Mhazini kwenye Kanda pamoja na viongozi wanaogombea kwenye mabaraza ya wazee, vijana na wanawake.

Juzi kamati hiyo ilikamilisha usaili kwa watiania wa nafasi za mabaraza ya chama hicho peke yake.