UTAFITI uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), umeonesha asilimia 5.8 ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) na kutumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.
Mtafiti Mwandamizi Kitengo cha Maikrobaiolojia na Kinga MUHAS, Dk. Doreen Kamori, aliyabainisha hayo juzi wakati wa Kongamano la 11 la chuo hicho lililoandaliwa kwa ajili ya kufanya tathmini ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya VVU na mapendekezo kukabiliana na tatizo hilo.
Dk. Doreen alisema walifanya utafiti huo mwaka 2020 katika mikoa 22 Tanzania Bara, ikiwamo Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.
Alitaja sababu zinazochangia tatizo hilo ni pamoja na kuingizwa nchini dawa ambazo zinachangia usugu na watu kutokuwa wafuasi wazuri wa kutumia dawa.
Alitoa ushauri kwa serikali wanapofikiria kubadilisha dawa au kuingiza nchini ni vyema kuweka miongozo na kufanya utafiti kufahamu wingi wa VVU kwa wagonjwa na kuangalia namna ya kuboresha.
"Ni vyema kuweka miongozo na kujiandaa vizuri kumudu tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya VVU au kudhibiti kabla ya dawa hizo kuleta madhara," alisema Dk. Kamori.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud, alisema kongamano hilo limetoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kukubaliana namna sahihi ya kukabiliana na tatizo hilo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupambana na VVU.
Alisema tatizo hilo linazidi kuongezeka kwa sababu WAVIU wanaendelea kutumia dawa maisha yao yote, hivyo ni muhimu kuweka mikakati, ikiwamo kufuata maelekezo ya daktari na mwongozo unaotakiwa wakati wa kutumia dawa hizo.
Mtu anayeishi na VVU, anapaswa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu kutoka kwa daktari badala ya kutumia dawa kiholela. Hii itasaidia kukabiliana na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA).
"NIMR inatekeleza Mpango wa Taifa Kudhibiti Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza, yakiwamo maambukizi ya VVU na UKIMWI, tunatekeleza afua mbalimbali katika mapambano hayo ili kuwasaidia kuboresha maisha yao na kuchangia nguvu kazi ya taifa," alisema Prof. Said.
Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, alisema asilimia 4.5 ya watu wazima nchini sawa na watu 1,548,000 nchini, wanaishi na VVU. Kati ya hao, wanaotumia dawa, asilimia tano tayari wana usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA).
Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS Idara ya Fedha, Mipango na Utawala, Prof. Erasto Mbugi, alisema wanafanya makongamano kama hayo ili kufanya tathmini ya gharama mtu au jamii anayoipata kutokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Alisema kuwa bila kuweka mikakati ya kupambana na tatizo hilo, wananchi wataendelea kutumia gharama kubwa kutibu usugu wa vimelea hivyo dhidi ya dawa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED