TAHARUKI imezuka katika vijiji vinne vilivyoko Kata ya Kisiriri, wilayani Iramba, mkoani Singida, baada ya kuibuka vikundi vya kimila, maarufu Nkiri, vinavyodaiwa kutoza faini ya ng'ombe, mbuzi au fedha, na asiyetoa hutengwa katika shughuli za kijamii.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini vikundi hivyo vina safu za viongozi wake na mwananchi asiyetoa faini hiyo, hutengwa na kijiji au kitongoji na haruhusiwi kwenda dukani kununua bidhaa yoyote.
Kadhalika, haruhusiwi kwenda kusaga nafaka wala kwenda katika huduma za afya kupata matibabu na hawaruhusiwi kuhudhuria msiba utakapotokea katika eneo anamoishi na atakapofiwa hakuna atakayemfariji na atakayeonekana kafanya hivyo naye anatozwa faini.
Imebainika pia kuwa vikundi hivyo ambavyo vipo kila kijiji na kila kitongoji, vina sheria zao walizojiwekea, viongozi wa maeneo husika wakidaiwa ni sehemu ya wanufaika wa fedha zinazotozwa, hivyo kushindwa kuchukua hatua.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii kwa takribani miezi miwili, umebaini tatizo hilo ambalo limegeuka kero kubwa kwa wananchi ambao kila wanapolalamika, hakuna hatua zinazochukuliwa.
Uchunguzi umebaini wananchi wanaokubali kutoa ng'ombe au mbuzi, mifugo hiyo huchinjwa na nyama kugawanywa kwa watu wote wa kijiji au kitongoji husika.
Mmoja wa wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Mzee Wilfred Tuntuma, ambaye alisema ametozwa faini ya ng'ombe watatu baada ya kutuhumiwa kuhusika na tukio la mauaji ya Daudi Kitonka lililotokea Agosti 30, 2023.
Tuntuma alisema kuwa baada ya tukio hilo la mauaji kutokea katika Kijiji cha Kinalilya, walikamatwa watuhumiwa 10, akiwamo yeye, lakini Mei 13, 2024, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ilimwachia huru baada ya kubaini hakuhusika na mauaji hayo.
Alisema kuwa baada ya kurejea kijijini kwake, viongozi wa kikundi cha Nkiri, walimtaka alipe faini ya ng'ombe hao, lakini amekataa kutoa kwa sababu mahakama imebaini hakuhusika na mauaji hayo.
Tuntuma alisema viongozi wa kikundi hicho licha ya kuwapatia nakala ya hukumu ya mahakama inayoonesha kutohusika kwake katika mauaji hayo na nakala nyingine kuzipeleka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kinalilya na kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisiriri, wameshikilia msimamo wa kumtaka alipe faini hiyo.
Mzee huyo alisema kuwa baada ya kushikilia msimamo wa kukataa kutoa faini hiyo, ametengwa na jamii na haruhusiwi kwenda kununua mahitaji yoyote katika maduka matatu yaliyoko Kitongoji cha Shigani ambako anaishi.
Kadhalika, alisema amekatazwa na jamii kwenda kusaga katika mashine iliyoko katika kitongoji hicho na hivi karibuni kulipotokea msiba wa Nakembekwa Mathayo, alipohudhuria alifukuzwa na viongozi wa kitongoji.
Tuntuma alisema kuwa kutokana na kutengwa na jamii, hivi sasa anaishi kama yuko kisiwani na maisha yake yako hatarini, "kwa kuwa imefika wakati wananitishia maisha".
Kutokana na hali hiyo, Mzee Tuntuma ameomba serikali ngazi ya wilaya kuingilia kati suala hilo.
Alisema wenzake tisa aliokamatwa nao katika kesi ya mauaji, ndugu zao walibanwa na kikundi hicho na walitoa faini ya ng'ombe mmoja wakiwa gerezani na kuchinjwa na nyama kugawiwa kijijini.
KAULI YA MTENDAJI
Mtendaji wa Kata ya Kisiriri, Sihaba Mohamed, alikiri kutambua vikundi hivyo vilivyoko katika vijiji vya kata hiyo ambavyo ni Kisiriri, Kisimba, Kisana na Kinalilya vinavyotoza faini wananchi.
Alisema vikundi hivyo vya kimila vina sheria zao ambazo zinatekelezwa katika kila kijiji na kitongoji ambapo mtu akifanya tukio lolote tofauti na taratibu zao, huitwa na kupigwa faini ya ng'ombe, mbuzi au fedha.
"Ukifanya kosa halafu ukapigwa faini, mfano wanasema ‘tunataka ng'ombe watatu au mbuzi mmoja’, ukigoma kulipa, wanasema ‘wamekusamehe’, lakini baada ya hapo hutaruhusiwa kusaga nafaka katika mashine. "Kama kuna duka hutaruhusiwa kununua vitu, ukifiwa hawajui na hata kupewa lifti katika pikipiki hutaruhusiwa.
"Suala hili ni changamoto, labda kama inawezekana viongozi wa ngazi ya mkoa waingilie kati ili vikundi hivyo vivunjwe.
"Hii wilaya (Iramba) ina kata 20 na katika kila kata Nkiri ipo, labda tukae katika Kamati ya Ulinzi na Usalama tuongee suala hili. Katika kata yangu kuna vijiji vinne na vyote vina vikundi hivyo," alisema Mohamed.
Kuhusu madai ya Mzee Ntutuma, Mtendaji huyo alisema kuwa Septemba 3, 2024 aliwaita viongozi wa kikundi anakotoka mzee huyo kuongea nao na kukubaliana apunguziwe adhabu badala ya ng'ombe watatu, atoe mmoja.
Ni faini inayopendekezwa dhidi ya mzee huyo ilhali Mahakama Kuu ilishasema hana hatia ya mauaji.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, alipotafutwa na Nipashe jana, alisema serikali inaendelea kufuatilia mambo hayo ambayo alisisitiza yako kinyume cha sheria za nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED