Ulega aahidi kuimarishwa ulinzi, usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:35 PM May 14 2024
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
Picha: Bunge
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara itaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi.

Ulega aliyasema hayo leo  bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2024/25.

"Katika mwaka 2023/2024, hadi kufikia Aprili, Sekta ya Uvuvi imezalisha jumla ya tani 472,579.34 za mazao ya uvuvi. Kati ya hizo, tani 429,168.39 ni kutoka maji ya asili na tani 43,410.95 ni kutoka ukuzaji viumbe maji."

Amesema hadi kufikia Aprili 2024, uzalishaji wa mazao ya ukuzaji viumbe maji umefikia tani 43,410.95 kutoka tani 33,525.46 za mwaka 2022/23.

"Jumla ya tani 41,271.07 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572 wenye thamani ya Shilingi bilioni 515.78 waliuzwa nje ya nchi na kuingizia Taifa mrabaha wa Shilingi bilioni 14.44 ikilinganishwa na tani 29,466.98 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 150,308, wenye thamani ya Shilingi bilioni 453.80, waliouzwa nje ya nchi na kuingizia Taifa mrabaha wa Shilingi bilioni 12.56 katika mwaka 2022/2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.05 la mazao ya uvuvi yanayouzwa nje ya nchi." amesema Ulega.

Ulega amesema hadi Aprili 2024, jumla ya ng’ombe 2,957,724 na mbuzi/kondoo 2,828,248 wenye thamani ya Sh. trilioni 3.4, waliuzwa katika minada mbalimbali nchini ikilinganishwa na ng’ombe 2,218,293 na mbuzi/kondoo 2,121,187, waliokuwa na thamani ya Sh trilioni 1.7 waliouzwa katika mwaka 2022/23.

Aidha, amesema uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 803,264.3 mwaka 2022/2023, hadi tani 963,856.55 mwaka 2023/2024, ikiwa ni sawa na ongezeko la asimilia 16.7.