BAADA ya malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara kuhusu tozo na utaratibu wa ukusanyaji mapato Bandari za Kigoma kuwa chanzo kikuu cha mianya ya rushwa ambayo huleta hasara kwa serikali, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula, ametoa ufafanuzi kwamba hakuna upotevu wowote.
Jumatano ya wiki hii, katika kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa kilichofanyika ukumbi wa Lake Tanganyika, mkoani hapa, baadhi ya wajumbe walilalamikia utaratibu wa ukusanyaji wa mapato katika Bandari ya Kibirizi iliyoko Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuwa chanzo kikuu cha mianya ya rushwa ambayo huisababishia hasara serikali.
Walisema makusanyo mengi ya tozo hayaingii serikalini kwa kuwa yanatozwa holela bila mpangilio maalum.
Akizungumza jana na mwandishi wa habari hii kuhusu malalamiko hayo, Mabula alisema kimsingi hoja iliyowasilishwa katika baraza hilo ilihusu kuondolewa kwa tozo ya bandari ya Dola 10 ambayo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) haitozi.
“TPA haina tozo ya Dola za Kimarekani 10 wala Dola tano. Malalamiko ya Dola 25 hadi 30 yanaashiria kuwa mteja wa aina hiyo anakuwa amekutwa na ukiukwaji wa taratibu za sheria na hivyo hulipa kama hongo ili kuepuka adhabu na huo sio utaratibu,” alisema.
Mabula alisema malipo yote hutolewa risiti halali na iwapo kuna yanayofanyika bila risiti halali, mteja anasisitizwa kutoa taarifa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria.
“Hakuna upotevu wowote wa mapato unaotokea katika Bandari za Kigoma, tozo na makusanyo yoyote yapo kisheria na yamekuwa yakifanywa kwa kuzingatia sheria na taratibu za bandari,” alisema Mabula.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, alizielekeza taasisi zinazohusika kuangalia uwezekano wa kuhuisha mifumo na taratibu zao, ili ikiwezekana tozo zote zikusanywe sehemu moja.
Alisema malalamiko ya Ahaji Mabie juu ya utolewaji wa Dola 25 hadi 30 hauendani na uwezo wa wadau wa eneo la Kibirizi na hauko katika mwongozo wowote wa tozo za taasisi za serikali zinazofanya kazi bandarini.
Katika mkutano huo, Alhaji Mabie, mfanyabiashara kutoka kampuni ya usafirishaji wa mizigo na abiria Aifola, alisema abiria wanaosafiri kwa kutumia meli za mizigo zilizoidhinishwa ili kupunguza changamoto za usafiri kuelekea nchini Congo, hutozwa kati ya Dola 25 hadi Dola 30 kama malipo ya tiketi, japo hawapewi tiketi za mashine ya EFD.
“Bado wahusika wanatumia teknolojia ya zamani. Abiria hawakati tiketi katika mfumo maalumu, kinachofanyika wanaandikwa majina na mtu wa meli, wanatozwa Dola 25 au Dola 30 kisha anazichukua mtu anayekata tiketi na hakuna sehemu yoyote inayoonesha asilimia za tozo zinazoingia serikalini. Serikali iongeze usimamizi izuie mianya ya rushwa,” alisema Mabie.
Alisema fedha nyingi zinapotea akitoa mfano wa fedha za udongo kiasi cha Dola tano zinazolipwa na wageni kutoka nchini Congo pindi waingiapo nchini ambazo hazina risiti wala maelezo yoyote, jambo linalofanya serikali ipoteze mapato mengi kupitia lango la uchumi na biashara la bandari.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED