VILIO, simanzi vimetawala wakati wa kuaga miili ya wanakwaya watano wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Wazo, Dar es Salaam, waliofariki dunia juzi katika ajali ya gari, eneo la Kirinjiko, Same, mkoani Kilimanjaro.
Wanakwaya hao walifariki dunia wakati wakienda kumzika mwanakwaya mwenzao, Machame, wilayani Hai, Kilimanjaro aliyefariki siku nne zilizopita wakati akijifungua.
Wanakwaya hao ni Stephen Temba, Auleria Swai, Neema Ngusi, Charles Mchome na Maderina Mtenzo. Mbali na wanakwaya hao walipoteza maisha, wengine walijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same, Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mawenzi na Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC.
Ibada ya kuaga miili ya wanakwaya hao iliongozwa na Mkuu wa KKKT na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) Dk. Alex Malasusa, akisaidiwa na wakuu wa majimbo na wa dayosisi hiyo. Pia viongozi hao waliwaombea majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Askofu Dk. Malasusa alisema wamepokea kwa mshtuko tukio hilo la kusikitisha huku wakipokea pia salamu za pole mbalimbali kutoka kwa maaskofu, viongozi wa dini, serikali na watu binafsi.
“Jana tulipofika katika ibada tulisema tumegundua Mungu wetu si wa kawaida. Mungu akiamua jambo haliwezi kuzuilika. Tunapopanga mipango ya kuishi, tujipatie moyo wa hekima na hekima ni kumjua Mungu na kuamini yupo.
“Msiba huu utupe moyo wa hekima. Wanadamu wengi tunahangaika na kuwaelimisha watoto ili wafanye vizuri katika masomo lakini tunasahau kumwomba Mungu awape watoto wetu mioyo ya hekima.
“Kuishi maisha ya ibada lakini ninamwomba Mungu atupe moyo wa hekima kama Daudi anavyotwambia Mungu atujulishe kuzihesabu siku zetu tupate moyo wa hekima. Basi tujibwage kwa Yesu kwa kuwa hatujui siku wala saa atakayotuita,” alisema.
Katika ibada hiyo, aliwasifu wanakwaya hao walifariki dunia kwa kupenda ibada na kwamba ni washindi mbele ya Mungu na walifanya kazi nzuri ya kumtukuza kupitia uimbaji.
Wasemaji wa familia kwa pamoja waliwashukuru watu mbalimbali waliowakimbilia katika kipindi chote cha msiba pamoja na kanisa kwa kuendesha ibada ya kuwaaga ndugu zao.
Familia ya Madelini Mtenzi ilisema: “Tunatoka shukrani kwa kanisa la Usharika wa Wazo, madaktari wa Same waliopokea miili ya ndugu zetu na majeruhi wengine. Mungu awabariki.”
Msemaji wa familia ya Aurelia Swai, alilishukuru kanisa hilo huku akisema mpendwa wao watamsafirisha kumpeleka Moshi kwa ajili ya maziko yatakayofanyika keshokutwa.
Naye msemaji wa familia ya Neema Ngusi alisema hana maeneno mengi zaidi ya kumshukuru Mungu kwa kilichotokea.
Msemaji wa familia ya Stephen Temba aliushukuru uongozi wa kanisa hilo kwa kuwakimbilia katika msiba huo.
“Tunashukuru wote mliofika hapa kutuunga mkono. Mmeacha familia zenu asanteni sana. Familia ya Temba tunatoa shukrani hata kwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika (wa Wazo, Herman Kiporoza). Mungu ampe moyo huo hata kwa matukio mengine. Pia tunawashukuru ndugu, jamaa na marafiki wote kwa kutukimbilia,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED