SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: Walioko mahabusu waanika madhila

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:29 AM Jun 17 2024
Picha ya mahabusu.
Picha: Mtandao
Picha ya mahabusu.

WATOTO wanaokutwa na makosa ya kukinzana na sheria wanakabiliwa zaidi na jinai ikiwamo ubakaji, ulawiti, mauaji, wizi na uvutaji bangi na sigara.

Hayo yalielezwa jana na watoto wanaopewa malezi na marekebisho ya tabia katika mahabusu ya watoto iliyoko Upanga, jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
 
 Wakizungumza kupitia ngonjera, watoto hao walisema chanzo ni malezi duni ya familia, huku wakieleza kuwa ndani ya mahabusu hiyo wanapata ushauri, unasihi na mafunzo ya ujuzi yanayowawezesha kuwa raia wema wanaporejea uraiani.
 
 Watoto hao walisisitiza umuhimu wa elimu jumuishi kwa watoto wote izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi.
 
 Baadhi ya watoto ambao wamefanyiwa marekebisho ya tabia na sasa wako uraiani, walisema mabadiliko ya tabia yamefanya jamii iwakubali na kuwaamini baada ya kutoka mahabusu.
 
 Mwanaisha Nasoro alisema alifikishwa katika mahabusu hiyo Septemba mwaka jana na alitoka mwezi uliofuata baada ya kesi yake kumalizika, akiwa amepata ujuzi wa kushona nguo ambao anautumia hivi sasa.
 
 "Ninatoa wito kwa watoto na vijana wenzangu kwamba wafanye kazi kwa bidii na wasichague kazi, mradi ni kazi halali na waache tamaa hata kama wanalipwa ujira kidogo. Wasione aibu kufanya kazi au vibarua halali," alisema.
 
 Mwanaisha alishauri wazazi na walezi kupunguza kupiga watoto mara kwa mara kwa kuwa wanajenga usugu kwa watoto wao.
 
 Richard Felix alisema kuwa akiwa mahabusu, alifundishwa namna bora ya kuishi na jamii, jambo ambalo limemfanya akubalike aliporejea uraiani.
 
 "Sasa ninamsaidia mama yangu kazi zote za nyumbani. Ninajua kupika, kulima, kufanya usafi na zaidi nina tabia nzuri. Ninashauri vijana tujifunze kuwajibika na tuepuke makundi," Felix alisema.
 
 Chacha Marwa alisema alikaa mahabusu hiyo kwa miezi minne na nusu kwa kosa la jinai na sasa amekuwa raia mwema baada ya kufanyiwa unasihi.
 
 "Sasa hivi ninalima na ninaishi nyumbani kwa amani. Ninashukuru viongozi wa hapa kwa namna walivyonisaidia kurekebisha tabia yangu," alisema.
 
 Hata hivyo, Chacha alisema anakabiliwa na changamoto ya kiuchumi baada ya hali mbaya ya hewa kuharibu mazao yake shambani.
 
 Naye Nuru Abdallah alishauri vijana kuwasikiliza wazazi na kuepuka makundi.
 
 Awali Meneja wa Mahabusu hiyo, Darius Damas, alisema watumishi kituoni huko wanafanya kazi ya kurekebisha watoto tabia kwa kuwafanya wajutie makosa yao, wabadilike na wakubali kuwajibika katika jamii.
 
 Alisema takwimu zinaonesha kwamba watoto wa kiume ndio wanaokabiliwa zaidi na makosa kulinganishwa na wa kike.
 
 "Mahabusu ina uwezo wa kuhudumia watoto 50 wa kiume na wa kike 10, lakini tangu nimeanza kazi hapa miaka mitano iliyopita, hatujawahi kuwa na watoto sita wa kike kwa mara moja. Hata leo tuna watoto 13 na miongoni mwao wa kike ni mmoja tu," alisema Damas.
 
 Meneja huyo alisema changamoto kubwa ya kuwafanya watoto wakinzane na sheria ni malezi duni ndani ya familia, ikiwamo kuwanyima baadhi ya haki za msingi kama vile chakula.
 
 Alisema mahabusu inakabiliwa na miundombinu mibovu ya majitaka na majengo yake kuezekwa mabati ya asbestos yaliyopigwa marufuku, hali inayohatarisha afya zao.
 
 Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Yassin Masenga, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, alisema wazazi na walezi wanapaswa kusimamia wajibu wa malezi ya watoto kimwili na kiroho ili kuwaepusha kulelewa na mifumo mingine.
 
 Alisema desturi ya maisha na elimu ya dini ni maarifa ambayo familia zinapaswa kuwafundisha watoto mapema ili wakue wakimjua Mungu.
 
 Kuhusu changamoto za mahabusu, alisema JMAT kwa kushirikiana na wadau wake itazifanyia kazi.
 
 Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni 'Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.' 

Sheria ya Ulinzi wa Mtoto ya Mwaka 2009, pamoja na mambo mengine, inaelekeza wazazi, walezi na jamii kuhakikisha watoto wanapewa haki zao za msingi ambazo ni pamoja na elimu, chakula, kucheza na kudekezwa.