WAZIRI WA Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema serikali itapeleka Sh.milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati yenye hadhi ya kituo cha afya ndani ya eneo la uchimbaji madini ya Tanzanite la Mirerani.
Kero ya kukosekana huduma za afya eneo la uchimbaji iliibuliwa na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka wakati wa mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC,Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM,Amos Makalla ambaye yupo kwenye ziara kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama,kusukiliza kero za wananchi,kuangalia uhai wa chama na kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
Makalla alimpigia simu Waziri Mchengerwa akimweleza kero ya wananchi kuwa wanaomba wajengewe zahanati yenye hadhi ya kituo cha afya ili wachimbaji na wafanyakazi wengine wakiugua au kuumia wapate huduma za afya.
"Tunategemea kutoka kwako namna ya kuwasaidia hawa wananchi wenye mapenzi mema na Rais Samia Suluhu Hassan," alisema.
Mchengerwa alisema dhamira ya Rais Samia ni kuona Watanzania wanapata huduma za afya kwa karibu na kwamba yeye kama msimamizi wa afya ya msingi atawaelekeza wataalam kwenda kufanya tathimini na Katibu Mkuu kutenga fedha Sh.mil 200 kwa ajili kuanza ujenzi wa majengo.
Aidha,Mchengerwa aliahidi kutembelea eneo hilo na kwamba fedha itatengwa kwa mwaka huu wa fedha ili wananchi wapate huduma kwenye makazi yao au wanapofanyia kazi,na kwamba ni lazima watekeleze kwa kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Alisema Ilani ya Uchaguzi 2020-2025 imetekelezwa vizuri na kwamba hakuna awamu kama ya Rais Samia ambaye amepeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo.
"CCM ina wajibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi,hata kama tunakwenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Nawaaminisha changamoto zilizopo zitatatuliwa na CCM,"alisema.
Makalla ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, amesema katika ziara kwenye mikoa 17 wamebaini kwamba CCM ni imara kuliko wakati wowote,na kwamba kimeendelea kuaminiwa kutokana na sera na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
"Haijitaji kutumia akili nyingi kuonyesha vyama vingine vimepoteza mwelekeo ndio maana kila kukicha wanahamia CCM,hapa nimepokea wanachama 50 wenye kadi za kisasa,"amesema.
Makalla amesema kwa mfumo wa uchaguzi Tanzania ili ushike dola ni kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 27,2024 na Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED