RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema ameamua kujigeuza ‘chura’ kutosikiliza kelele zinazopigwa kwa kuwa anachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi na si kingine.
Amesema hajawahi kusikia Waziri wa Fedha amesifiwa bali siku zote analalamikiwa, hivyo kumtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, kwamba na yeye ategemee hivyo.
Rais Samia aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, katika hafla ya kupokea gawio kutoka kwa kampuni binafsi ambazo serikali ina hisa na kupokea michango kwa mujibu wa kisheria kutoka kwa mashirika na taasisi za umma. Hafla hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Mimi kazi mliyonipa ninasimama na kuifanya, lakini mnashuhudia matusi ninayotukanwa. Mpuuzi hana maana, huyu bibi eeeh! ana hivi. Mambo tele lakini ninajigeuza nani? Chura.
“Kulikuwa na mashindano ya chura wamewekewa mlingoti wakaambiwa atakayefika juu ana zawadi. Vyura wakaanza kupanda mmoja mmoja. Sasa huku chini watazamaji wakawa wanawaambia nyie mtaanguka shukeni, ninyi hatari hiyo hamwezi kufika shuka mtashindwa tu.
“Kelele nyingi kama zinazopigwa humu ndani kwenu. Kwa hiyo vyura wakaanza kushuka mmoja mmoja kabakia mmoja tu. Akapanda mpaka juu akaenda na akateremka. Kama kawaida wakaanza kumzonga umewezaje kufika, kumbe yule chura hasikii.
“Kwa hivyo zile kelele zote alizopigiwa yeye kapanda juu na mlingoti wake na mimi nimejigeuza vivyo hivyo chura. Kelele nyingi zinapigwa wakiona hujibu wanasema tulitukane atajibu. Sijibu nageuka chura sisikii kabisa. Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi hii, sitaki kingine,” alisema.
Rais Samia aliwaambia watendaji wa mashirika hayo kwamba kwenye mageuzi watakanyaga ‘nguru wa mshihiri’ huku akiwaonya anayetaka kumkera amkanyagie uchumi wake.
“Lakini katika mageuzi haya tutakanyaga wengi wale ambao hawataki kwenda mbele na ndio wataopiga kelele nyingi sana. Sasa ndugu yangu mwanangu wewe kwenye shirika ambaye hutaki kukanyagiwa nguru wako, nenda kachape kazi.
“Leta mageuzi kwenye shirika lako, chapa kazi tuone tija. Hatutakanyaga nguru wako kama unanikanyagia mimi nguru wangu wa uchumi na mimi nitamkanyaga wako. “(Kwenye) kelele tujigeuze chura, tuzibe masikio tupande mti mpaka tukishuka ndiyo tutasema hivi mlikuwa mnasemaje vile? Lakini letu limeshakuwa,” alisisitiza.
Pia aliwaonya wanaofanya kazi kwa mazoea na kutaka wabadilike na kufanya kazi kwa faida ya nchi, huku akifurahishwa na mashirika ambayo yamepiga hatua na sasa yanajilipa mishahara bila kutegemea serikali.
MASHIRIKA KUSOMANA
Rais Samia alisema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amezungumzia wale wanaoogopa mageuzi kwa hofu.
“Mwaka wa tatu ninapiga kelele mifumo kusomana, lakini mtu akiangalia kimrija kitakatika anasema bado. TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania) mmeanza ninawashukuru mnasomana na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) lakini ninataka muwe mnasomana kamili,” aliagiza.
Aliyataka mashirika mengine kufanya hivyo, huku akimwagiza mtu wa hazina anayesimamia mashirika ahakikishe hesabu zao zinasoma kinachoingia na kutoka kionekane.
Pia alimweleza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali (mstaafu) Venance Mabeyo, kwamba Ngorongoro inaweza kusimama yenyewe.
KELELE BANDARI KUUZWA
Rais Samia alipongeza kampuni zilizotoa gawio serikalini na mashirika yaliyotoa mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mujibu wa sheria.
“Kama TPA, mwaka jana kiwango chenu hakikuwa hivi, lakini kwa mageuzi yaliyotokea bandarini, mmeweza kufikia kiwango hiki na mwakani tunatarajia kiwango kikubwa zaidi pengine mara mbili ya hiki.
“Hakuna sababu kama mtajiendesha na sekta binafsi iliyoko pale kuna watu wawili ambao tumeshawaruhusu mmeomba maombi zaidi lakini hata wale wawili tu kwa mwakani mnaweza kuongeza hii mara mbili.
“Na huko ndiko tulikuwa tunaelekea ndugu zangu. Wale mliokuwa mnapiga kelele Mama kauza bandari, mauzo yale faida yake ni hii na huu ni mwanzo na tunatarajia tutapata faida kubwa zaidi kwa bandari zetu zote kubwa,” alisema.
Rais alisema serikali imepokea hisa kutoka kampuni 10 zilizochaguliwa na hiyo ni fursa muhimu ya kukutana hapo kupeana changamoto.
Aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuvuka kiwango baada ya utendaji na usimamizi mzuri wa mapato huku TASAC (Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania), BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) zikitakiwa mwakani zifanye vizuri zaidi.
Rais aliitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutafuta chanzo kingine cha mapato badala ya kutegemea mkaa ambao ana vita nao.
ASIFU MAGEUZI
Pamoja na mashirika mengi hayajatoa migawo yao, Rais alisifu mageuzi yanayoendelea huku akiagiza wenyeviti kuendelea kuyasimamia ili nayo kutoa magawio.
“Tumeambiwa na Msajili wa Hazina hapa kwamba makusanyo bado yanaendelea. Lengo letu kwa mwaka huu ni Sh. bilioni 850 na sasa wako kwenye Sh. bilioni 600 na zaidi. Ni imani yangu mliobaki mtachangia au mtaleta gawio lenu ili tufikie lengo tulilojiwekea,” alisisitiza.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED