RC Shinyanga asistiza maombi kwa Taifa, Rais

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:50 PM Apr 24 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia) akizungumza wakati wa kufungua semina ya Waadventista Wasabato.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia) akizungumza wakati wa kufungua semina ya Waadventista Wasabato.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewasisitiza viongozi wa dini mkoani humo, kuendelea kuliombea Taifa amani, pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, ili Mungu aendelee kumpatia maono mazuri ya kuongoza nchi katika kweli na haki.

Amebainisha hayo jana wakati akifungua semina ya familia, malezi, biashara na huduma za afya, ambayo inaendeshwa na Kanisa la Waadventista Wasabato, ukanda wa dhahabu – ‘Nyanza Gold Belt Field’ (NGBF).

Amesema nchi ikiendelea kuwa na amani na maendeleo yanapatikana, na hivyo kuwasihi viongozi wa dini kwamba katika ibada zao au mikutano ya maombi mbalimbali wasisahau kuliombea Taifa, Rais pamoja na wasaidizi wake akiwamo Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

“Kanisa la Waadventista Wasabato tuzidi kuliombea Taifa letu kuwa na amani, sababu amani ni ya Mwenyezi Mungu, pia tumuombee na Rais wetu Samia ili Mungu aendelee kumpatia maono mazuri ya kuliongoza Taifa kwa haki na kweli, sababu haki ikitendeka amani inapatikana,” amesema Macha.

“Tukiwa na amani nchi yetu itakuwa na maendeleo, na hakuna Taifa lenye maendeleo kama hakuna amani, hivyo nawasihi pia viongozi wote wa kidini, kila siku, tuendelee kuombea amani ya nchi yetu,” ameongeza Macha.

Aidha, amelipongeza kanisa hilo, kwa kuendesha semina hiyo ambayo inathamani kubwa kwa taifa, kwa kutoa masomo ya familia na makuzi, afya pamoja na Biashara.
Amesema kanisa hilo limekuwa likijitoa sana katika kuhakikisha makuzi ya vijana, yanakuwa katika msingi wa maadili mema, kwani kwa sasa kuna janga la mmomonyoko wa maadili kwa vijana, hivyo semina kama hizo zisipotolewa Taifa linakosa vijana wenye maadili.

Kwa upande wa masomo ya afya Anamringi ameitaka jamii kuzingatia lishe bora, sababu magonjwa mengine hasa yasiyo ya kuambukiza, husababishwa na mtindo mbovu wa maisha, na kwamba kupitia mafunzo hayo, yanaijenga jamii yenye afya bora.

Aidha, wafanyabiashara kuwa na hofu ya Mungu, na kufanya biashara zao kwa haki bila ya ‘kuchakachua’ bidhaa, pamoja na kulipa kodi halali ya Serikali.

Naye Askofu wa jimbo la NGBF, Enock Sando, amesema kanisa hilo limeendelea kujipambanua ulimwenguni kote na kugusa jamii, kuisaidia kujitegemea kupitia semina za biashara ili wakristo wawe na fikra chanya na hivyo kujikwamua kiuchumi sababu Mungu hapendezwi na umaskini.

Kwa upande mwingine, Askofu huyo amesema kuwa kanisa hilo lina amini katika afya bora, kwani bila watu kuwa na afya bora, hakuna maendeleo.