SIMANZI, majonzi na vilio vimetanda kuanzia usiku wa jana Januari 13,2025, kwenye kata ya Segera, wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kufuatia vifo vya watu 11 na majeruhi 13, kutokana na ajali ya gari.
Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ametuma salaam za rambirambi kufuatia vifo hivyo, kutoa pole na kuwatakia kupona haraka majeruhi wa ajali hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian, pamoja na kuwasilisha salaam za Rais Dk. Samia, amesema ajali hiyo imesababishwa na roli la mizigo lenye namba T 782 BTU.
Amesema, roli hilo liliacha barabara na kuelekea mahali walipokuwa watu wakiwaokoa majeruhi kutoka kwenye gari nyingine iliyotokea awali, ikilihusisha gari aina ya Tata lenye namba T 720 EJP.
Kwa kujibu wa Balozi Dk. Batilda, gari hilo kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, lililobeba abiria ambao idadi yao haijajulika, lilipinduka kwenye kijiji cha Chang'ombe, hivyo wakazi wake na wale wa kijiji jirani Cha Maili Kumi, kwenda kushiriki uokozi.
Wakiwa katika kutekeleza azma hiyo, Balozi Dk. Batilda anasema, ndipo roli hilo likisadikiwa kukata breki, lilipoteza mwelekeo na kwenda eneo waliokuwa wanakijiji wanaokisiwa kufikia 50 na kuwagonga baadhi yao.
Mganga wa Mfawidhi wa Hospitali ya Magunga - Korogwe, Dk. Paul Patrick amethibitisha kupokea miili ya watu 11 na majeruhi 13.
Amesema hadi kufikia leo asubuhi, miili nane ilikuwa imetambuliwa wakati majeruhi saba wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo kwa matibabu zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED