Rais Samia ateua viongozi mbalimbali usiku huu, yumo Dk. Akwilapo
By
Mwandishi Wetu
,
Nipashe
Published at 02:28 PM Oct 31 2024
Picha:Mtandao
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi tisa usiku huu leo Oktoba 30,2024 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, uteuzi huo umejumuisha viongozi wafuatao:
Dk. Leonard Douglas Akwilapo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Dkt. Akwhilapo, ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu, anachukua nafasi ya Prof. Penina Mlama aliyemaliza muda wake.
Prof. Zacharia Babuu Mganilwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Prof. Mganilwa, Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anachukua nafasi ya Dk. Naomi Katunzi aliyemaliza muda wake.
Dkt. Mwamini Madhebehi Tulli ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA). Dk. Tulli anahudumu kwa kipindi cha pili.
Mhandisi Dk. Richard Joseph Masika ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Dk. Masika anachukua nafasi ya Prof. Henry Mahoo aliyemaliza muda wake.
Balozi Salome Thaddaus Sijaona ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU). Balozi Sijaona ameteuliwa kwa kipindi cha pili.
Prof. Joseph Nicolao Otieno ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Prof. Otieno, ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), anachukua nafasi ya Prof. Hamisi Malebo aliyemaliza muda wake.
Janet Reuben Lekashingo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini. Kabla ya uteuzi huu,Lekashingo alikuwa Kamishna wa Tume ya Madini na sasa anachukua nafasi ya Prof. Idris Kikula ambaye amemaliza muda wake.
Asha Dachi Mbaruk ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Magazeti Tanzania (TSN). Hapo awali, Mbaruk alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Mariam Salehe Mgaya ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji kwenye Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI). Kabla ya uteuzi huu, Mgaya alikuwa akikaimu nafasi hiyo.