Prof. Nombo: MUHAS Mlonganzila kuwa mji wa mafunzo ya Afya

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 07:17 PM Jun 27 2024
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema serikali inajenga Mji wa Mafunzo ya Afya (Academic Medical City) katika Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Prof. Nombo ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 12 la Kisayansi la Chuo hicho ambapo amesema serikali inaendelea na mikakati ya kupanua miundombinu stahiki katika Kampasi hiyo kupitia utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Ameongeza kuwa Serikali inajenga na kukarabati majengo zaidi ya 130 kwa ajili ya kuboresha mazingira na kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji katika Elimu ya Juu ambapo Miongoni mwa miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa kampasi kubwa ya MUHAS Mkoani Kigoma.

"Serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha na kujenga miundombinu stahiki katika Kampasi hii. Kupitia kazi hizi kubwa za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali yetu,wadau mbalimbali wametukimbilia na kuamua kutushika mkono na kama Serikali daima tunathamini washirika wetu amesisitiza Prof. Nombo.

Makamu Mkuu Wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa.
Akizungumzia Kongamano hilo, Katibu Mkuu amesema kuwa Serikali inaelewa umuhimu wa wanasayansi kukaa pamoja na kujadili na kubadilishana maarifa ya kisayansi ambayo yataboresha hali ya utoaji huduma za afya na afya za wananchi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema majadiliano ya aina hiyo husaidia Serikali katika kuboresha Miongozo ya matibabu, kuandaa taratibu na mbinu za kinga dhidi ya magonjwa.
Mwenyekiti Wa Baraza La Chuo, Dkt Harrison Mwakyembe.
Aidha matokeo ya mojadala yatasaidia watunga Sera na Wanasayansi, na kubaini changamoto na kuzipatia ufumbuzi wa kisayansi.

Aidha, amewataka wanasayansi kujadili na kutoa mapendekezo kwenye maeno ya njia mpya za kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya afya ya akili,, kisukari, moyo, saratani na matumizi ya teknolojia kwenye afya hasa kwenye upande wa Akili Bandia (Artificial Intelligence).

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema kuwa MUHAS imeendelea kuwa kitovu cha kutegemewa na Taifa kwa matokeo ya tafiti za afya.