Prof. Aboud awapa ushauri wanaotumia dawa za kufubaza VVU

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:47 PM Sep 04 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) Prof. Said Aboud

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) Prof. Said Aboud ametoa ushauri kwa watumiaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi kuhakikisha wanafuata maelekezo ya daktari ili kuepukana na tatizo la usugu wa dawa.

Prof. Aboud ametoa ushauri huo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kongamano la Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Amesema kuwa mtu ambaye atatumia dawa kiholela na asiyefuata maelekezo ya daktari husababisha kirusi cha Ukimwi kujenga usugu mwilini.

“Mgonjwa anatakiwa kutumia dozi ya dawa kwa makini kwa kuzingatia maelekezo ya daktari, akitumia kiholela yule mdudu kirusi cha Ukimwi anapata fursa ya kujenga usugu dhidi ya ile dawa anayotumia na matokeo yake ni kushindwa kufanya kazi,” amesema.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo wa Muhas, Profesa  Emmanuel Baladya amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa juhudi zao kuhakikisha wanashirikisha wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na sehemu nyingine kuangalia ni wapi wamefika katika kushughulikia tatizo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) Prof. Said Aboud.
Profesa Baladya, amedai kuwa karibu asilimia tano ya wanaotumia baadhi ya dawa, wana usugu ambapo pia, wapo wanaotumia dawa haziwasaidii na asilimia 90 wamegundulika wana usugu.

Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa  MUHAS,  Dk. Doreen Kamori amesema mwaka 2020 walifanya utafiti katika mikoa 22 kuangalia ukubwa wa tatizo la usugu wa dawa za kufubaza na kupunguza makali ya VVU na kugundua wenye usugu wengi ni wale walioko kwenye matibabu.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo wa Muhas, Profesa Emmanuel Baladya.

Amesema dawa mojawapo inayojulikana duniani kuwa ni nzuri sana  iliyoingizwa nchini 2019  ya Dolutegravier licha ya kusifiwa kwa ubora na ufanisi wake wa kupunguza makali wamegundua ina  viashiria vya kuonesha kuna resistance dhidi ya dawa hiyo.

“Tunaona kama nchi tunapofikiria kubadilisha dawa au kuitambulisha katika nchi ni vyema kuweka miongozo na kujiandaa vizuri kwa kufanya tafiti kuangalia wingi wa virusi kwa watu walioko kwenye tiba na kujipanga taratibu kuingia kwenye dawa mpya, kuwafuatilia watu wanaoishi na virusi kubaini kama zina changamoto,”amesema.

Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa MUHAS, Dk. Doreen Kamori.