Mvua yazidi kuleta maafa

By Grace Mwakalinga ,, Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:16 AM Apr 24 2024
Maafa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
PICHA: MAKTABA
Maafa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

MVUA inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, imesababisha maafa ikiwamo kuharibika kwa miundombinu, makazi ya watu kuzingirwa na maji na baadhi ya huduma kusimama.

Mitandao ya kijamii imeonyesha baadhi ya barabara za Dar es Salaam zikiwa zimejaa maji na kusababisha usafiri katika maeneo hayo kusimamishwa. 

Aidha, baadhi ya barabara magari yalipita kwa taabu huku yale madogo yakishindwa kupita kwa sababu ya kujaa maji. Miongoni mwa maeneo hayo ni Shoppers Plaza, Mikocheni, Dar es Salaam ambako maji yalijaa barabarani. 

Taarifa zaidi zilieleza kuwa mvua hiyo inayonyesha katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwamo ya pwani, imesababisha uharibifu mkubwa wa mindombinu ikiwamo ya uchukuzi. Baadhi ya mikoa hiyo ni Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.         

WANAFUNZI WAKWAMA 

Zaidi ya wanafunzi 80,000 wa shule za msingi katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, wamekosa masomo kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki, ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kujionea athari za mvua hizo katika shule na makazi katika wilaya za Rufiji na Kibiti ikiwamo kuharibu miundombinu ya elimu.

Ziara hiyo ilijumuisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda na Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo.

Amesema shule 11 za msingi zenye wanafunzi 7264 wakiwamo wasichana 3657 na wavulana 3607 wameathirika na mafuriko wilayani Rufiji.

Aidha, amesema nyumba 58 za walimu pia zimeathiriwa na kupoteza samani na mali zilizokuwamo ndani ya nyumba hizo.

Amesema katika Wilaya ya Kibiti wanafunzi 824 katika shule saba za msingi zimeathirika huku tatu zikifungwa kutokana na adha hiyo huku sekondari ya Mtanga Delta ikiathirika pia.

“Athari za mvua ni kubwa zimeharibu miundombinu ya shule na wanafunzi kukosa sehemu za kusoma, mkoa umefanya jitihada kuhakikisha wanakuwa salama na kuainisha shule ambazo hazijaathirika na mafuriko ili zipokee wanafunzi kuendelea na masomo,” amesema Sara.

Akizungumzia maafa hayo, Waziri Prof. Mkenda, amesema serikali imeweka utaratibu kwa wanafunzi wote waliokumbwa na mafuriko hayo kusoma kwenye shule maalum ambazo zimetengwa.

Mkenda amesema mwanafunzi yeyote asibaki nyumbani kwa sababu ya mafuriko na badala yake wazazi wawapeleke kwenye shule ambazo zimeainishwa na viongozi wa maeneo hayo.

Kuhusu miundombinu amesema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga mabweni, vyoo, madarasa, vifaa vya kufundishia na chakula kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu.

Amesema tayari wizara imetoa baadhi ya vifaa vikiwamo vitabu vya kiada na ziada, madaftari na penseli na kalamu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Muhoro na Katundu ambazo ni miongoni mwa zinazopokea wanafunzi walioathirika na mafuriko.

Katibu Mkuu Prof. Nombo, amesema wanaendelea kufanya tathmini ya athari za mafuriko katika sekta ya elimu, lakini amepongeza jitihada za walimu kuendelea kuwapo kwenye vituo vya kazi na kufundisha licha ya mafuriko.

Akifafanua kwa wanafunzi wa madarasa yenye mitihani amesema serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha wote wanatambulika na kurudi shule.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema timu ya wataalam imeweka kambi kuhakikisha wananchi wote waliokumbwa na mafuriko wanahamishiwa kwenye makambi maalum, ikiwamo ya Nyamwage ambayo imewekwa kwa ajili ya kutoa huduma zote muhimu.