MNEC CCM Rukwa atofautiana na serikali kufungwa uvuvi Ziwa Tanganyika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:36 PM Jun 27 2024
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif

Wakati Serikali ikiwa imefunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif, ameruhusu wananchi kuendea la shughuli hizo.

Seif alitoa kauli hiyo jana (June 26, 2024)  wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ninde, Kata ya Ninde wilayani Nkasi mkoani humo.

Itakumbukwa kuwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, akitangaza lengo la Serikali la kufunga kwa muda shughuli za uvuvi alisema lengo ni kupumzisha  shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.

Kauli za Seif zilizonukuliwa katika video fupi inayozunguka mitandaoni, ikimnukuu MNEC  huyo  akihamasisha wananchi kuendea na shughuli za uvuvi,  inatofautiana na sababu zilizotolewa na Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdala Ulega ambaye alisema uamuzi wa Tanzania unatokana makubaliano yaliyoazimiwa katika kikao kilichofanyika mwaka 2022 kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ulega alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Aliongeza uamuzi huo unatokana na utafiti uliobainisha kuwa kumekuwepo na upungufu mkubwa wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika kunakotokana na ongezeko kubwa la uvuvi usio endelevu uliopelekea uharibifu wa mazalia ya samaki.