WANAFUNZI zaidi ya asilimia 90 wanaosoma katika Shule ya Msingi Makorora na Azimio jijini Tanga wapo katika hatari kubwa ya kugongwa na pikipiki, magari na vyombo vyengine vya moto, na ili kuwanusuru Shirika la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswis wamejenga miundombinu salama ya barabara ili kuwawezesha kuvuka kwa usalama.
Hayo yamebainishwa leo Mei 29,2024 jijini Tanga wakati wa uzinduzi wa mradi wa Miundombinu salama ya barabara katika shule hizo ambapo viongozi wa ngazi mbalimbali wa Wilaya ya Tanga wamehudhuri huku wakionesha kufurahishwa na utekelezwaji wa mradi huo.
Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema takribani wanafunzi wanane katika shule hizo katika kipindi cha mwaka mmoja wamejeruhiwa kutokana na ajali za barabara zinazotokea kwa kukosekana alama za barabara na maeneo ya vivuko.
“Baada ya kushauriana na wadau wa shule hizo wakiwemo wanafunzi na walimu, jamii, viongozi wa dini, serikali za mitaa,TARURA) na Jeshi la Polisi , hivyo Amend kwa ufadhili Uswisi na tumeshirikiana kutekeleza mradi huu kwa kuweka vivuko pamoja na alama muhimu za barabarani," amesema.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo wameweka njia za waenda kwa miguu, matuta, vivuko vya pundamilia, alama za barabarani, na elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wote.
"Tumezindua miundombinu mipya ya kuokoa maisha ya watembea kwa miguu hasa watoto katika shule hizi," amesema.
Amesema katika Bara la Afrika watoto wako katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani ikilinganishwa na eneo lingine lolote duniani na kufafanua bahati nzuri njia za kuzuia ajali hizo zinaeleweka.
Amesema mradi huo unaungwa mkono na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na una bajeti ya Sh. Milioni 424.9 huku akifafanua mradi ulianza Septemba mwaka 2023 na shughuli zilizofanyika ni mafunzo kwa madereva bodaboda 300 katika Jiji la Tanga.
Pia madereva bodaboda 253 katika Jiji la Dodoma sambamba na kampeni ya uhamasishaji kuhusu masuala ya usalama wa pikipiki pamoja na kuanzishwa kwa 'Kanuni za Maadili' kwa waendesha pikipiki 200 ambao watapewa mafunzo jijini Tanga ifikapo Juni 2024.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED