MIAKA 3 YA SAMIA: Aenda na staili ya vitendo kuliko maneno mengi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:31 AM Mar 13 2024

UNAPOSIKIA kwenye vyombo vya habari kwa nchi yoyote, kiongozi wa taifa, kama vile rais ni mwanamke, kitu gani kinakujia kichwani? Ni mtazamo wa jinsi au jinsia?

Kwa nchi za kiafrika, Tanzania ikiwamo, kuwa kiongozi mwanamke, kuna mitazamo tofauti katika jamii ama hasi au chanya. Pamoja na dhana hizo, wako wanawake waliozishinda. 

Rais Suluhu Hassan, ni mmoja wa marais saba (kwa mujibu wa tovuti ya africa.com) wanawake waliotia fora barani Afrika. Kati yao wako walioingia Ikulu, japo kwa mpito yaani miezi michache tu, huku sita wakishika madaraka kamili. 

Alipotwaa tu madaraka, ujumbe wake ulikuwa: “Na hapa naomba niseme tu kidogo, kwa wale ambao wana mashaka. Mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais.”

Viongozi hawa wanawake, wameweka historia barani Afrika na duniani kote, huku dunia ikiendelea kupambana na nafasi za wanawake viongozi ili kufikia 50/50. Nia hasa ni kuvunja mkwamo wa kijinsia na kuwa na uongozi shirikishi wenye usawa.

Machi, 2021 Rais Samia alitangazwa rasmi na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha Rais John Magufuli. Akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa juu zaidi katika historia ya nchi ya miaka 63 ya uhuru hivi sasa.

Kimataifa, kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, 2021 na 2022, ametajwa na taasisi za kimataifa likiwamo jarida la Forbes kuwa miongoni mwa viongozi wanawake 100 (Forbes: The World's 100 Most Powerful Women-2021) wenye ushawishi duniani.

Kadhalika mwaka 2022, taasisi ya kimataifa ya Avance Media, iliwatambua wanawake kutoka Afrika kupitia mradi wa kuwawezesha wasichana ‘Be A Girl’ ikiwatambulisha Wanawake 100 Waafrika Wenye Ushawishi Zaidi (100 Most Influential African Women), Samia akiwamo.

Mengi aliyoyafanya Rais Samia, yamo anayoyabeba kama kiongozi yeyote bila kujua jinsi, ingawa kwa tafsiri nyingine moja kwa moja, anabebwa na sura zote, akisimama kama kiongozi, mwanamke na mama.

Usemi kwamba ‘Mcheza Kwao Hutuzwa’. Huu unalenga kuwapa moyo na hamasa waliofanya vizuri. Rais Samia, aliwarejeshea tabasamu mabinti waliokatiza masomo wakiwa shuleni kutokana na sababu tofauti lakini kubwa zaidi ni ujauzito.

Akiibeba ajenda ya dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 2030), aliwahamasisha wasichana kurejea masomoni baada ya kujifungua. Mabinti hao ni kati ya wale ambao walikuwa na ndoto ya kuwa kama mwanamke fulani na kuiongoza jamii kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa.

Rais Samia anafuata mkondo wa kauli za awali kutoka viongozi wa kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Irina Bokova, mwaka 2017 alisema elimu ya mtoto wa kike ni muhimu katika kusaidia kutimiza malengo ya SDG ifikapo mwaka 2030 ambalo ni  lengo namba nne linalohusu elimu.

“Bila kuhusisha wasichana katika elimu, bila kushughulikia vikwazo muhimu katika elimu yao kama ubaguzi, vikwazo vya umaskini, ukabila na dini, hatuwezi kufikia uendelevu katika malengo yoyote ya elimu na malengo mengine ya maendeleo endelevu,” anasema. 

Rais Samia, katika baadhi ya mambo aliyoyatazama kwa ukaribu na kwa jicho la kijinsia, ni kufanikisha elimu ya juu na kuwafikia wote, kwa kutenga Sh. bilioni 70 zaidi ya Sh. bilioni 500, kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mkopo kwa ajili ya elimu ya juu mwaka 2021.

Pia alitangaza kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kwa kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito, kurejea masomoni huku akiongeza vyumba vya madarasa na kutenga Sh. bilioni 125 kwa ajili ya kukamilisha maboma 10,000 mwaka huo.

AVUNJA DHANA 

Wakati akielekea kutimiza miaka mitatu Machi 19, mwaka huu, tangu aapishwe kuwa Rais, Nipashe inamwangazia kwa namna tofauti, ikiwamo mtazamo wa jinsi na jinsia, akivunja dhana hasi zilizotopea miongoni mwa wanajamii.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Samia alieleza mambo mengi, bila kuacha kuirejea kauli aliyojitamkia awali hadharani na umma kumshangilia. 

Katika mahojiano mwishoni mwa wiki iliyopita, Samia alitaja hatua alizopitia hadi kukifikia kiti cha urais, akianzia jimboni kuwa mwakilishi Makunduchi, Kisiwani Zanzibar na itaja namna ilivyokuwa changamoto jamii kumpokea.

“Wakati wa lile tamko, nilikuwa nimekumbuka kutiana moyo katika mambo ya maisha. Unajua wanaume wanapofanya jambo na akielekea kushindwa, anaambiwa ‘mrume’ hujikaza, nenda nenda, kwa hiyo na mimi sikuile, nikasema hapa 'mrume' hujikaza.

“Bila kujua au kuwa na uhakika naenda kufanya nini, nikasema nisimame. Niwahakikishie Watanzania kwamba aliyesimama hapa ni rais wa Tanzania, na nimesema vile nikijua changamoto iliko na wasiwasi ulioko mioyoni kwa watu.

“Ni mara ya kwanza kupatwa na hali ile tuliyokuwa nayo…wengi waliingiwa na hali ya ‘shock’ (mshtuko), lakini anayeingia angekuwa ‘jibaba’ mwenye misuli angalau kidogo wangetulia. Lakini anaingia mwanamke mwenye vishungi vyake, anasema kwa wepesi zaidi, na anatizama kama hataki.

“Nadhani wasiwasi mkubwa zaidi ulikuwa kwenye watu. Ile ilikuwa ndiyo changamoto yangu ya kwanza, nina msiba, lazima nivuke salama na aliyemama lazima aonyeshe kwamba nchi inaweza kuvuka. Ule ulikuwa mtihani wangu wa kwanza. Siyo siri mara ya kwanza niliposhika madaraka joto nililisikia,” alisema.

Anaikumbushia kauli hiyo kila mara na walioko kwenye hadhira huinuka  kumshangilia, kwa tafsiri nyepesi kwamba ‘yaliyomo yamo’, jinsi na uongozi, kwenye jamii za Kiafrika kuna neno.

“Na watu walilipuka kwa shangwe, kwamba kweli tumepata rais…kilichonisukuma kusema...ni tayari kulikuwa na minong’ono ataweza kweli huyu hebu angalieni, inawezekana.

“Rais haina ‘gender’ (jinsi), rais ni rais tu. Mamlaka  ni mamlaka tu. Hofu isingeacha kuwapo kwa watu wote, kwanza kupoteza rais aliyekuwa madarakani, pili mwanamke anaingia pale, ku-re-place."

Anafafanua tangu dhamira yake iliyokuwapo awali moyoni mwake, akipenda kuwa mhudumu wa kwenye ndege (air hostess) na dhamira yake ikikatizwa na baba yake, aliyetamani bintiye airithi taaluma yake ya ualimu.

“Enzi zetu wakati huko shule, wala huwazi utakuwa nani nilikuwa naona ATCL (sasa ATCL)… ukiona ‘airhostess’ wanavyovaa, wanapendeza kweli, nikatamani kuwa kama wale, lakini masomo yangu yalikuwa sayansi.

“Lakini baba yangu mzazi alikuwa mwalimu. Nilipomaliza  kidato cha nne, akanipangia kwenda ualimu lakini usiku uleule, nikatoroka baadaye nikawa karani. Nakumbuka nilikuwa mfano wa kupewa adhabu shuleni…ili iwe mfano kwa wengine,” anasema. 

MARAIS BARANI

Katika Afrika, wako marais tisa waliofikia hatua kama ya Rais Samia, wakishika mamlaka ya kuiongoza nchi kwenye nchi zao, wakiweka historia na rekodi, kwa jicho la dhana ya jinsi na jinsia.

Kwa nchi za Kiafrika, mgawanyo wa majukumu hutofautiana kulingana na jinsia kwamba mwanamke jukumu lake ni kama vile kupika, kuteka maji, wakati jinsi, ni tofauti za kibaolojia ambazo majukumu yake hayaingiliani, mfano mwanaume hawezi kubwa jukumu la ujauzito.

Marais hawa walitia fora wakiziongoza nchi zao, huku vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, wakiwaangalia kila uchao, yale wanayoyamudu, kwa kuwa wengi wao nchini mwao ni mara ya kwanza kuwa na kiongozi mwanamke. 

Ellen Johnson Sirleaf, akiwa Rais wa Liberia kuanzia Januari, 2006 hadi Januari 2018, ni mmoja wa wanawake hao. Mwingine ni Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, bado yumo madarakani kuanzia Oktoba mwaka 2018 hadi sasa.

Yumo pia Ameenah Gurib-Fakim, aliyekuwa Rais wa Mauritius, kuanzia Juni mwaka 2015 hadi Machi mwaka 2018. Mwingine Catherine Samba-Panza, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Januari, 2014 hadi Machi, 2016.

Joyce Banda wa Malawi, naye aliweka rekodi akishika madaraka kwa nchi hiyo tangu Aprili mwaka 2012 hadi Mei mwaka 2014. Sylvie Kinigi, alishika madaraka akiwa Rais wa mpito wa nchi ya Burundi, kuanzia Oktoba, 1993 hadi Februari, 1994.

Agnès Monique Ohsan Bellepeau, alikuwa rais pia wa mpito wa Mauritius, tangu Machi, 2012 hadi Julai, 2012 na Mei mwaka 2015 hadi Juni 2015. Rose Francine Rogombé, alikuwa Rais wa mpito nchi ya Gabon, kuanzia Juni mwaka 2009 hadi Oktoba 2009.