Mfumo wa e-Board wapunguza gharama uendeshaji vikao Ilemela

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:14 PM Apr 24 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma (e-Board).

Matumizi ya Mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma (e-Board), umetajwa kurahisisha uendeshaji wa vikao na kupunguza gharama za maandalizi katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Ilemela ndiyo halmashauri ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo wa e-board kati ya halmashauri 184 nchini, ambao umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Akizungumza kuhusu mfumo huo ofisini kwake jijini Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela  Ummy Wayayu, amesema kuwa kabla ya halmashauri hiyo kuanza kutumia mfumo wa e-Board mwaka 2023, fedha nyingi zilikuwa zinatengwa katika ununuzi wa shajara,wino na vifaa vingine kwa ajili ya vikao vya madiwani na menejimenti.

“Kwa mwaka tulikuwa tunatumia takribani shilingi milioni 200 hadi 300 katika maandalizi ya uendeshaji wa vikao, lakini kwa sasa gharama hizo hatuna tena kwakuwa tunatumia  mfumo huu wa e-Board, ambao umetusaidie kupeleka fedha hizo katika mambo mengine ya muhimu katika halmashauri,” amesema.

Ameongeza kuwa, mfumo wa e-Board umesaidia kupunguza gharama za kudurufu taarifa mbalimbali na badala yake zinapakiwa kwenye mfumo na madiwani wanapakuwa na kuendelea kuzifanyia kazi.