MBUNGE wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu, amehoji serikali imejipangaje katika kudhibiti matukio ya wizi wa watu au utekaji nchini.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mbunge huyo alisema mkoa wa Iringa ni moja ya waathirika na matuko hayo na wamepoteza vijana wawili, Banis Nyato na Ali kwa kutekwa.
Kutokana na swali hilo, Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson alimtaka Mbunge kuwasilisha swali hilo kama swali la msingi ili serikali itoe majibu kikamilifu.
Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege, alihoji lini wizi wa mifugo utadhibitiwa wilayani Rorya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, alisema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kudhibiti wizi wa mifugo katika wilaya ya Rorya.
Alisema jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi ni pamoja na kutoa elimu juu ya ulinzi jirani, kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi na mazizi salama.
“Juhudi zingine ni kuimarisha kikosi cha kupambana na wizi wa mifugo (STPU ) kwa kuongeza askari na vitendea kazi, kufanya mikutano ya ujirani mwema na polisi wilaya ya Nyatike ya nchini Kenya juu ya udhibiti wa makosa yanayovuka mipaka na jitihada zote hizi ni endelevu na zimepunguza kwa kiasi kikubwa wizi wa mifugo,” alisema.
Hata hivyo, alisema takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Desemba, 2023 na mwezi Januari, 2024 kumeripotiwa matukio 26.
Pia alisema kwa kipindi kama hicho Desemba, 2024 na Januari, mwaka huu, matukio hayo yamepungua na yaliyoripotiwa ni tisa ikilinganishwa na mwaka uliopita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED