KATIBU wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amewataka wananchi kuwaogopa na kuwakataa wanasiasa wanaopandikiza chuki kwa lengo la kuligawa taifa.
Makalla pia amewahakikishia Watanzania kuwa CCM kama chama kiongozi, itahakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na haki; atakayeshinda ndiye atakayetangazwa.
Akizungumza jana na wananchi wa Monduli katika eneo la Mto wa Mbu wakati wa mkutano wa hadhara, Makalla alisema ni muhimu wananchi wakaelewa kuwa maandamano hayajengi shule wala zahanati, bali ni kupoteza muda.
Alisema kuna wanasiasa wanaeneza chuki kuwa wafugaji watahamishwa na hawatakiwi nchini, jambo ambalo alisisitiza ni uongo ambao haupaswi kusikilizwa.
"Hatuna Tanzania nyingine, tusikubali kugombanishwa na watu ambao wana malengo yao, tutunze amani yetu kwa nguvu zote, Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda wafugaji ndio maana ameleta miradi mingi ya maendeleo," alisema.
Makalla alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia uhai wa chama, kukagua utekelezaji Ilani ya CCM 2020-2025, kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Wakazi ili wawe na sifa ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Makalla alisema kuwa katika mikoa 17 waliyotembelea wamejiridhisha kuwa uhai wa chama uko vizuri na wana uhakika wa kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
"CCM haihitaji mbeleko, utekelezaji ilani yetu ni kielelezo tosha cha kurudi kwa wananchi... ukitembea kila mahali nchini kuna alama ya miradi ya maendeleo inayoachwa na Rais Samia, yote inawahusu wannachi, hivyo hatuhitaji kubebwabebwa bali tunajibeba wenyewe," alisema Makalla.
Katibu huyo alisema CCM kama chama kiongozi watahakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na kwamba atakayeshinda kwa haki ndiye atakayetangazwa na si vinginevyo.
"Ni muhimu kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wanachagua viongozi wenyeviti wa vitongozi, kijiji, mitaa ambao ni muhimu sana. Matumaini tuliyonayo fedha za miradi zinapokuja zipate watekelezaji," alisema.
Alisema serikali imeshusha fedha nyingi za maji, zahanati, shule na kwamba ni muhimu watenge siku moja kati ya Septemba 11 hadi 20 mwaka huu 2024 kwenda kujiandikisha ili kupiga kura Novemba 27 mwaka huu.
"Wana CCM, mashabiki wa CCM, wasio na vyama ila wapenda maendeleo wajitokeze ili tumpe nguvu Rais Samia ambaye amethibitika ni mzalendo pekee anayeleta maendeleo, kila unapopita kuna alama ya mradi wa darasa, kituo cha afya, mradi wa maji, yote yamefanywa na serikali ya CCM," alisema.
Alisema ni muhimu vijiji 62 na vitongoji 230 viwe kijani (CCM), na kwamba chama hakitapitisha wagombea ambao watakilazimu kutumia dodoki na sabuni kuwasafisha.
"Mimi ndio msemaji wa chama, CCM itawaletea wagombea safi, wazuri wasio na makandokando kuja kufanya kazi nanyi, hatutaleta wagombea wanaoleta migogoro, wasiosoma taarifa za matumizi bali safi wanaostahili," alisema.
Alisema kuwa baadhi ya vyama vimekuwa vya matukio na havina wajibu wala dhamana kwa wananchi, bali CCM ndio yenye jukumu la kuleta maendeleo.
Alikosoa maandamano ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), akidai hayajaleta maendeleo, bali yalikuwa ya kujidhururisha na kuwataka wananchi kutodanganyika.
"Wenzenu wanawaandamanisha wanapata posho, nyie mnaandamana bure na kuambiwa mkunje ngumi, CCM ina wajibu, ni chama kiongozi kitakachowaletea maendeleo," alisema.
Makalla alidai CHADEMA haina uwezo wa kushinda uchaguzi, bali inapotokea wameshinda ni kwa sababu kuna mgogoro ndani ya CCM.
Katika mkutano huo, Makalla alipokea kero 51 za wananchi 42, ikiwa ni pamoja na wananchi wawili kutoingizwa katika orodha ya wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) licha ya kuwa na sifa, ubovu wa barabara na shida ya maji
Pamela Ijumba Ofisa Kilimo Wilaya ya Monduli, akijibu baadhi ya kero, alisema kero ya mfereji kujaa matope itafanyiwa kazi baada ya uboreshaji skimu ya umwagiliaji, huku watendaji wengine wa serikali wakieleza mkakati wa kuzitatua kero zilizowasilishwa.
Baada ya ufafanuzi wa watendaji wa serikali, Makalla alisema CCM inawajibika na kero za wananchi na kwamba baada ya kupokea muhtasari wa namna kero za wananchi zitakavyotatuliwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, atawapigia mmoja baada ya mwingine kujua kama kero hizo zimetatuliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED