Maaskofu wakemea ndoa za jinsia moja

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:25 AM Apr 01 2024
 Mkuu wa Jimbo la Tumaini na Usharika wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mufindi, Mchungaji Baraka Mbangula akipokea zawadi ya mshumaa kutoka kwa marafiki zake toka nchini Ujerumani waliofika kanisani kushiriki Ibada ya Pasaka.
PICHA: FRANCIS GODWIN
Mkuu wa Jimbo la Tumaini na Usharika wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mufindi, Mchungaji Baraka Mbangula akipokea zawadi ya mshumaa kutoka kwa marafiki zake toka nchini Ujerumani waliofika kanisani kushiriki Ibada ya Pasaka.

KATIKA kuadhimisha misa takatifu ya sikukuu ya Pasaka, maaskofu katika maeneo mbalimbali nchini wamekemea vikali vitendo vya kikatili vinavyosababishwa na imani za kishirikina dhidi ya watoto, wanawake na wazee.

Pia wamesisitiza suala la maadili katika familia ikiwa ni pamoja na kukemea na kudhibiti ndoa za jinsia moja zinazozidi kushamiri katika jamii. 

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, akihubiri katika Mkesha wa Pasaka uliofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, amesema pasaka ni kukombolewa kutoka kwenye utumwa wa dhambi.

Amesema Kristo alifia dhambi za wanadamu na kuifungua milango ya mbinguni ambayo ilikuwa imefungwa kutokana na dhambi, hivyo kuwataka watu kuacha kutenda maovu, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba.

"Tuuvue utu wa kale tuvae utu mpya, acheni uasherati, uzinzi, ushirikina, ugomvi, mauaji na kutoa mimba kwani yote ni machukizo kwa Mungu. Wakumbukeni pia yatima na wajane, mnapowatendea mema, mnamtendea Yesu Kristo,” amesema Askofu Sangu.

Ametumia misa hiyo kuliombea taifa pamoja na viongozi wote ili waendelee kudumisha na kusimamia amani hususani kuelekea uchaguzi wa ngazi mbalimbali na kuwaita waamini wenye sifa za kugombea nafasi hizo kuzitumia vizuri.

Pia amewataka Watanzania kutokudanganywa kwa rushwa katika kipindi cha uchaguzi na kupoteza haki zao, bali wapokee fedha na vitu hivyo na kuwaangusha katika sanduku la kula.

“Wakikuletea wewe pokea tu, weka mfukoni, kula lakini kwenye kura wapige chini. Hapa niwaombe wagombea wanaotumia rushwa kutafuta kura, huo si uzalendo, ni ubinafsi. Niwakumbushe wale wenye uwezo wa kugombea nafasi tumieni wakati huo kuonesha uwezo wenu ili kuzikomboa jamii zenu,” amesema.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa, akiongoza misa hiyo jana, amehimiza waumini tutokukaa katika giza la maisha pale wanapokumbana na matatizo mbalimbali katika maisha yao na kuhakikisha wanayakabilia kupitia maombi kwa Mungu. 

Pia amewataka kutokukata tamaa wakati wote wanapokumbana na majaribu, bali kupitia maombi kwa Mungu ili wayashinde na kupata ushindi wa milele.

“Tujifunze kutoka kwa Kristo mfufuka juu ya neema ya kupenda na kusamehe hata kutokukata tamaa mpaka pale alipotekeleza adhima yake ya kukomboa ulimwengu kutoka kwenye dhambi,” amesema Kardinali Rugambwa.

NDOA JINSIA MOJA

Askofu wa Jimbo Katholiki Bukoba, mkoani Kagera, Jovitus Mwijage amehimiza kinamama kuwa waombezi wa familia zao kutokana na wao kupewa kipaumbele cha kushudia ufufuko wa Yesu Kristo kaburini.

Askofu Mwijage amesema kwa neema hiyo na maagizo yaliyotolewa na Yesu Kristo wakati wa mateso yake, wanawake wanapaswa kuwa wasimamizi wazuri wa maadili na mienendo mizima katika familia, ndoa na watoto na kuwadhibiti kwenda kinyume cha maadili.

“Matukio mengi yanayokwenda kinyume cha maadili na imani ikiwamo mavazi yasiyofaa, kuvaa mavazi ya jinsia tofauti yanayoashiria vitendo vya mapenzi ya jinsia moja. Ukiona binti yako au kijana amevaa nguo ambayo si yake,  kaa naye umwonye, umrudishe katika mstari.

"Utaona sasa wavulana wametoboa masikio, wamevaa suruali iko chini, hiyo kwa nchi nyingine ukiona mtu amevaa hivyo, huyo anakuwa ni shoga, mkanye mtoto mapema,” amesisitiza Askofu Mwijage.

Askofu Mstaafu Jimbo Kuu Katoliki la Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini, pia amesisitiza umuhimu wa maadili mema kwa watoto, akihimiza kuwalea kwa kuzingatia mafundisho ya dini na kuacha kiburi ambacho kimekuwa kinasabisha kukosa heshima kwa wazazi na kufuata mambo yasiyofaa katika jamii.

“Lazima tukumbuke kuwa katika maisha yetu ya kila siku kitu kizuri kinalipa na vilevile kitu kibaya kinaharibu, hivyo jiandae kuharibu pale unapotenda mabaya na kulipwa pale unapotenda mema,” amesema Askofu Kilaini.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Antony Lagwen pia amekemea vitendo viovu vya ndoa za jinsia moja, ulawiti na ubakaji katika jamii, akisisitiza havikubaliki kwa mtu yeyote, vipingwe kwa nguvu zote.

"Ndugu zangu tusikubali kufumbia macho ushoga, ulawiti na ubakaji, tuvipinge kwa nguvu, mtu yeyote anayetaka twende huko tusimsikilize, amejaa uovu, bali tumkimbilie Yesu aliyefufuka leo," amesema.

Ni vitendo vilivyokemewa pia na Naibu Katibu Mkuu Misioni ya Uinjilisti ya Dayosisi ya Kaskazini Kati ya KKKT, Julius Laizer, ameyesema Watanzania wanapaswa kupambana na kupiga vita matendo machafu ya ushoga, usagaji, ndoa za jinsi moja, ulawiti na ukatili wa kijinsia.

MINDE NA USASA

Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Ludovick Minde, amesema kiini cha vijana wengi nchini kupoteza uwezo wa kufikiri, kusema, kushirikisha mambo, kutenda na mwenendo mzima wa maisha yao ni 'usasa' unaochagizwa na ukuaji wa sayansi na teknolojia.

"Kwa sasa wimbo uliopo duniani ni kuporomoko maadili kwa vijana na watoto. Je, sisi wazazi na walezi tumejitafakari nini chanzo cha haya?

"Jibu ni kila mmoja kushindwa kujifungamana na Yesu na badala yake kujikita katika mambo ya kidunia. Haifai, haipendezi, tubadilike!" Askofu Minde ameonya.

"Ninapotoa salama za pasaka, ninaomba niwaalike nyote kuwa wapya na kuyatafakari maisha yetu, tuache kuendelea na utandawazi na badala yake turudi nyumbani kwa Yesu Kristo, ili kufurahia matunda ya upendo, msamaha, ukweli na kuwa tayari kubebeana upungufu kwa ajili ya mwenzio.

"Haya mambo ya kulipiza kisasi, kuwaua watoto, ndugu na wazazi ili tupate fedha si yetu. Tubadilike tunakoenda siko," amehadharisha.

UCHAGUZI MITAA

Mkoani Iringa, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mufindi, Dk. Antony Kipangula ametaka Watanzania kuendelea kuomba ili Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu ufanyike salama, pia kuombea maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani ili kupata viongozi wenye hofu ya Mungu.

Katika salamu zake za Pasaka huko Mafinga, Askofu Kipangula amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu kwa nchi, hivyo lazima maandalizi yake yaende sambamba na maombi ili kupata viongozi wenye hofu ya Mungu.

Amesema uchaguzi huo utaunda serikali kwa ngazi za vijiji na mitaa, hivyo iwapo watapatikana viongozi wasio na sifa itakuwa mzigo Kwa taifa.

"Lazima viongozi wenye sifa wapatikane ili kuja kupata madiwani, wabunge na Rais mwenye hofu ya Mungu kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani," amesema na kutoa rai kwa wale wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali badala ya kuwa watazamaji na kuwaachia wale wasio na sifa.

Askofu Dk. Kipangula pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kuendelea kuchukizwa na vitendo vya ufisadi nchini.

Amesema ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambazo Rais Samia alikabidhiwa Alhamisi iliyopita, zimeonesha kiongozi huyo anachukizwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.

"Maagizo ya Rais Dk. Samia kwa wale wanaohusika na upotevu wa fedha za umma ni vyema yakafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na wahusika kuchukuliwa hatua kali," amesema.

Kuhusu dayosisi hiyo mpya ya Mufindi, amesema kwa sasa kanisa linaendelea kupanga vyema safu ya viongozi watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

* Imeandaliwa na Vitus Audax (MWANZA), Marco Maduhu (SHINYANGA), Restuta Damian (KAGERA), Oscar Assenga (TANGA), Allan Isack (ARUSHA), Mary Mosha (MOSHI) Steven William (MUHEZA), Mariam Bole (SAUT), Jaliwason Jasson (MANYARA), Elizabeth Zaya (DAR), Godfrey Mushi (MOSHI) na Rahma Suleiman (ZANZIBAR).