Lori laua watu 13 kwenye mteremko

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 09:49 AM Jun 06 2024
Baadhi ya wananchi wakishirikiana na Askari Polisi kuondosha moja ya pikipiki ambazo zilihusika kwenye ajali ya lori iliyosababisha vifo vya watu 13 majeruhi 18 katika mteremko wa Simike jijini Mbeya jana.
Picha: Nebart Msokwa
Baadhi ya wananchi wakishirikiana na Askari Polisi kuondosha moja ya pikipiki ambazo zilihusika kwenye ajali ya lori iliyosababisha vifo vya watu 13 majeruhi 18 katika mteremko wa Simike jijini Mbeya jana.

WATU 13 wamefariki dunia papohapo na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea jana kwenye mteremko wa Mbembela, jijini Mbeya.

Ni baada ya lori lililokuwa limebeba kokoto kufeli breki na kuparamia magari mawili, pikipiki na guta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Benjamin Kuzaga, akiwa eneo la tukio, alitaja lori lililosababisha ajali hiyo ni aina ya Scania lenye namba za usajili T. 979 CVV na tela lenye namba za usajili T. 758 BEU ambalo lilikuwa linatoka Uyole kuelekea Barabara ya Tunduma.

Alisema lori hilo liligonga gari dogo aina ya Harrier lenye namba za usajili T. 120 DEL na kupoteza mwelekeo kisha kugonga gari aina ya Coaster lenye namba za usajili T. 167 DLF lililokuwa linatokea Tunduma kwenda jijini Mbeya.

Alisema lori hilo liliparamia waendesha pikipiki, maarufu bodaboda, na guta ambalo lilikuwa limebeba mahindi.

Alisema vifo na majeruhi wengi ni waliokuwa katika gari la abiria ambalo liliburuzwa mpaka kwenye mtaro. Wengi wao walikuwa wamebanwa.

"Dereva wa lori tumempata na tunaendelea kufuatilia hawa wa vyombo vingine ili kubaini kama ni miongoni mwa majeruhi ama waliopoteza maisha, lile gari dogo aina ya Harrier kilichotokea ni uharibifu wa chombo," alisema Kuzaga.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia ajali hiyo walisema waliona gari hilo likiwa linashuka mlima huo likiwa limewasha taa na kupiga honi kuashiria hatari.

Mmoja wa mashuhuda hao, Bashiri Mwaluwanda alisema dereva wa lori hilo alifanikiwa kuyakwepa baadhi ya magari na bajaji kwenye mteremko huo na baada ya kugonga gari dogo, alipoteza mwelekeo na kuanza kuyumba.

Alisema kuwa baada ya kugonga basi dogo la abiria (coaster) na kuanguka walianza kuokoa baadhi ya waathirika hasa majeruhi na kuwakimbiza hospitalini kwa kutumia pikipiki na bajaji kabla ya magari ya kubeba wagonjwa kufika eneo la tukio.

Alisema kuwa baadhi ya watu ambao walikuwa wamebanwa kwenye basi dogo la abiria waliondolewa baada ya askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika na vifaa.

"Watu waliofariki (dunia) ni wengi, dereva wa lori amejitahidi sana kuyakwepa magari mengine na yaliyokuwa yanapandisha kwenye huu mteremko, yule wa coaster alishindwa kumkwepa kwa sababu ni eneo la matuta," alidai Mwaluwanda.

Mapinduzi Mwambambe, shuhuda mwingine wa ajali hiyo, alisema alipigiwa simu na mdogo wake ambaye anafanya shughuli zake eneo la Simike, akamweleza kwamba kuna lori limefeli breki linashuka uelekeo wa Mbembela na akamtahadharisha kama alikuwa barabarani, alipaswa kuondoka.

Alisema kabla mdogo wake hajamaliza kutoa maelezo hayo, alisikia kishindo barabarani na alipokwenda kuangalia akakuta lori hilo limeshagonga gari la abiria ndipo akaanza kushiriki uokoaji.

Alisema uokoaji ulikuwa rahisi kwa sababu ni eneo la jeshini na hivyo askari wengi wa kikosi cha Jeshi cha 844 Itende KJ walishiriki uokoaji pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo vingine vya dola.

Nipashe lilishuhudia magari manne ya kubeba wagonjwa, mawili ya Jeshi la Polisi na moja la Jeshi la Wananchi (JWTZ) yakisomba majeruhi na miili ya marehemu kupeleka katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya.