Lori la mchanga lagonga basi, laua abiria wanne

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:48 AM Jun 17 2024
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Willy Mwamasika.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Willy Mwamasika.

WATU wanne wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya lori kuligonga kwa nyuma gari dogo la abiria aina ya Nissan Caravan.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Willy Mwamasika, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo saa tatu usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Tanganyika, wilayani Muheza, mkoani Tanga.

Akizungumza na mwandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Maketi Msangi, alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha  basi dogo la abiria Nissan Caravan lenye namba T228 DTD  na lori aina ya Volvo lenye namba  T 925 CAU ambalo lilikuwa limebeba mchanga kuelekea mjini Tanga. 

Alitaja watu waliopoteza maisha ambao walikuwa abiria kwenye basi kuwa ni Kondakta Anuari Juma (30), Shani Omari na Hassan Abdallah (mmoja alikuwa hajatambuliwa) huku majeruhi wanne wakipelekwa kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Muheza.

Akifafanua kuhusu tukio hilo, Kamanda Msangi, alisema chanzo cha ajali ni basi dogo kupata hitilafu na kumlazimu dereva kulisimamisha pembeni.

Alisema kuwa wakati amesimama, anakagua basi hilo abiria waliteremka na kondakta wakawa wamesimama pembeni mwa basi hilo, ghafla lilitokea lori hilo likagonga basi kwa nyuma na kusababisha vifo na majeruhi.

Alisema dereva wa lori la mzigo, Elvice Livingston alitoroka baada ya ajali na kukimbilia kusikojulikana. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Teule Muheza.