TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)-Dar Group, imeweka kambi ya siku tatu ya upimaji wa magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza kwa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jimbo la Kati Usharika wa Kitunda Relini.
Upimaji huo umeanza jana, ni utekelezaji wa tiba mkoba ijulikanayo ‘Dk. Samia Suluhu Hassan Outreach Services’, imefanyika viwanja vya kanisa hilo, jijini Dar es Salaam.
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka JKCI-Dar Group, Dk. Samueli Rweyemamu, alisema: “Katika kambi hii tumekuja na daktari bingwa wa saikolojia, kuangalia afya ya akili kwani tatizo la afya ya akili limekuwa kubwa katika jamii.
“Watu wenye tatizo hilo, wakirudi kwa mchungaji wakapata huduma za kiroho, watakaa vizuri na kuepuka magonjwa kama shinikizo la damu,” alisema Dk. Rweyemamu.
Dk. Rweyemamu alisema lengo kuu la kambi hiyo ni kufikisha huduma katika jamii, kutoa ushauri wa namna ya kujikinga na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) na kutoa huduma za matibabu endelevu.
“Tunatoa huduma za kuchunguza na kutoa chanjo ya homa ya ini, kuchunguza na kutoa matibabu ya saratani na tezi dumu, kuchunguza na kutoa matibabu ya kisukari, shinikizo la damu na moyo.
“Kuchunguza na kutoa matibabu ya matatizo ya masikio, pamoja na kutoa huduma kwa watu wanaohitaji ushauri,” alisema Dk. Rweyemamu.
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa JKCI-Dar Group, Dk. Eva Wakuganda, alisema wazazi wakiwa na utaratibu wa kuwafanyia uchunguzi wa afya watoto wao, itasaidia kugundua matatizo ya kiafya, kumpa nafasi ya matibabu mapema.
“Kuna wakati tunakutana na changamoto za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo, unakuta mtoto alihitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo kabla hajafikisha mwaka mmoja, lakini kwa sababu mzazi hakugundua mapema anamleta mtoto akiwa na zaidi ya mwaka mmoja, hivyo kukwamisha baadhi ya matibabu,” alisema Dk. Eva.
Mkuu wa Jimbo la Kati KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Frank Kimambo, alitoa wito kwa waumini wa kuona umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya, ili washiriki kikamilifu katika kumtumikia Mungu, pamoja na shughuli za kiuchumi.
Alisema kati ya ibada zote zilizofanyika mwaka huu, hiyo imekuwa ibada kubwa, kwani waumini na wakazi wa kitunda wameweza kufikiwa na huduma za afya bila gharama, hivyo kuushukuru uongozi wa kanisa hilo.
“Nawashukuru madaktari bingwa wa JKCI, Ocean Road, Muhimbili na Hospitali ya Magereza Ukonga, kwa kuacha ofisi zenu na kuja kutuhudumia, Mungu amewapa uwezo kushughulika na miili hii, iliyoumbwa naye, ni sadaka kubwa sana mmeitoa kwa ajili yetu,” alisema Mchungaji Kimambo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED