WIZARA ya Katiba na Sheria, imezindua rasmi Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Huduma za Kisheria ambacho kitakuwa kinapokea malalamiko, hoja maswali na tuhuma za rushwa kwa njia ya simu kutoka kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kutatuliwa moja kwa moja na wataalamu.
Kituo hicho kimezinduliwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, hafla iliyoshirikisha viongozi wadau mbalimbali pamoja na wananchi na kwamba kituo hicho ni sehemu ya Kampeni ya Kitaifa ya Huduma za Kisheria ya Mama Samia.
Prof.Kabudi alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni miongoni wiazara vinara zinazotekeleza kwa vitendo falsafa za Rais Samia Suluhu Hassan za 4R, ambazo ni maridhiano, ustahilmilivu, mabadiriko na kujenga upya.
“Na kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, imefanikiwa kupita katika mikoa saba na hivi karibuni itaanza kuendelea katika mikoa mingine iliyobaki,”alisema Prof.Kabudi.
Alisema wizara imeanzisha kituo hicho baada ya kubaini kwamba malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakiwasilishwa wizarani kwa njia ya barua au kufika moja kwa moja kwenye ofisi za wizara kwa kutumia gharama kubwa za usafiri na kujikimu wakiwa Dodoma na kwamba uwapo wa kampeni hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, imesaidia kuleta hamasa kubwa kwa wananchi kuwasilisha malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria ambazo zinahitaji ufunbuzi wa haraka.
Alisema kupitia huduma hiyo, wananchi waliopo maeneo ya mbali kwa sasa wataweza kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya simu katika kituo hicho cha huduma kwa mteja cha huduma za kisheria teja na yakafanyiwa kazi kwa wakati bila mwananchi kulazimika kufika ofisi za wizara.
“Kituo hiki ni ishara ya maendeleo una udhibitisho wa dhamana ya kuwahudumia watanzania kwa bidii, uwazi na uadilifu, kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa mteja katika dhama hizi za teknolojia ni hatua muhimu inayohitajika katika kuboresha njia za serikali za kushirikiana katika utoaji wa huduma. Hii inaonesha kutambau kwetu kwa mahitaji yanayoendelea, matarajio ya wananchi pamoja jitihada zinazohitajika katika kukabiliana na changamoto zao.
“Juhudi hizi ni muhimu kwa kuwa wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo kituo hiki ni ishara ya wazi ya serikali kutumia njia rahisi za kiteknolojia kuwafikia wananchi ili waweze kuwasilisha changamoto zao ziweze kutatuliwa kwa ufanisi na kwa wakati, kituo kinafanya kazi saa zote za kazi na wizara inafikiria kuongeza muda kifanye saa 24 siku zote saba za wiki,”alisema Prof.Kabudi.
Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wizara ya Katiba na Shearia, Jane Lyimo, alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni pamoja ni pamoja na kuboresha mifumo ya mawasiliano na huduma kwa umma.
Kadhalika, alisema ni matokeo ya programu ya kujenga taasisi katika kupambana na rushwa inayotekelezwa na wizara hiyo kwa lengo maalumu la kuziwezesha taasisi ikiwamo wizara katika kupambana na rushwa Tanzania na inatekelezwa kwa kushirikiana na idara maalumu ambayo inaratibu na kusimamia kituo hicho kutoa Ofisi ya Rais Ikulu kupitia ufadhili wa serikali ya Uingereza ambayo imewezesha uanzishwaji wa kituo hicho.
Alisema kituo hicho ambacho kimezinduliwa kwa lengo la kupokea taarifa za rushwa, hoja na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi, kilianza kufanya kazi Februari 21 mwaka huu baada ya kukamilika kwa usimikaji wa mfumo na vifaa mbalimbali vya kiteknolojia ya kisasa.
“Kuna eneo mahsusi limetengwa kwa ajili ya kituo hiki na tangu kuanzishwa kwake kituo kimemeendelea kupokea malalamiko ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini na huduma zinatolewa na wataalamu mahiri ambao wamejengewa uwezo,”alisema Jane.
Alisema mafanikio yaliyopatikana tangu kianze kutoa huduma ni pamoja na kupokea malalamiko yanayohusu huduma za kisheria, kuratibu masuala ya kisheria kwa wasiomudu gharama za uanasheria, kupokea maoni, mapendekezo na ushauri uu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na wizara.
Alisema Kituo hicho kimefanikiwa kurahisishia wananchi kufuatilia utekelezaji wa malalamiko yao kwa wakati pasipo kulazimika kufuata huduma hizo wizarani na hivyo kupata nafasi za kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED