KILIO cha kikokotoo cha mafao ya wastaafu kimesikika, serikali imetangaza kuongeza mafao ya mkupuo baada ya kustaafu:
Watumishi ambao ni wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) sasa watapata mafao ya mkupuo kwa kikokotoo cha asilimia 40 badala ya asilimia 33 iliyoibua malalamiko.
Wenzao wa sekta binafsi walioko Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) nao wanatarajiwa kushuhudia ongezeko la mafao ya mkupuo, wakiwa na kikokotoo kipya cha asilimia 35 badala ya asilimia 33 iliyopo kisheria hivi sasa.
Kusudio la kuwa na kikokotoo hicho kipya cha mafao ya wastaafu lilitangazwa jana na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alipowasilisha bungeni mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha, huku Rais Samia Suluhu akifuatilia mubashara.
Waziri wa Mwigulu alisema kumekuwa na kilio kikubwa kutoka kwa wastaafu kuhusu kikokotoo cha sasa cha asilimia 33 kwa mifuko yote miwili - PSSSF na NSSF.
Kabla ya kikokotoo cha asilimia 33 kuanza kutumika mwaka jana, watumishi wa umma walikuwa na kikokotoo cha asilimia 50 na wale wa sekta binafsi walikuwa na chao cha asilimia 25.
"Kama asemavyo Naibu Waziri wa Fedha, (Hamad Hassan) Chande, kuwa mara zote 'mtoto akilia mama hujua kwa sauti kuwa hapo mtoto analilia nini.
"Akilia anasema hapo ameshiba, akilia anasema hapo ana usingizi, akilia anasema hapo nguo zimembana au akilia anasema apelekwe hospitalini'," alisema.
Waziri Mwigulu alisema serikali ni sikivu, imesikia kilio hicho na imekifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wastaafu na wanaotarajiwa kustaafu.
"Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliyopo hivi sasa hadi asilimia 40. Hili ndio kundi kubwa la watumishi wanaofanya kazi nzuri sana kwa taifa letu wakiwapo walimu, kada ya afya, polisi, magereza, uhamiaji, zimamoto na makundi mengine yaliyoko Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa," alisema.
Kwa kundi ambalo awali lilikuwa linapokea asilimia 25 (NSSF), serikali inapendekeza kupandishwa kwenda asilimia 35 kuanzia mwaka ujao wa fedha.
"Watumishi walioathirika na mabadiliko haya watazingatiwa katika mabadiliko haya. Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya wastaafu kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mifuko," alisema.
Dk. Mwigulu pia alisema serikali imeendelea kuhakikisha malimbikizo ya kimshahara na yasiyo ya kimshahara ya watumishi wa umma yanalipwa kwa wakati. Kwa miaka mitatu, Sh. bilioni 98.63 zimelipwa kama malimbikizo ya watumishi wa umma.
SURA YA BAJETI
Waziri Mwigulu alisema kuwa kwa mwaka 2024/25, serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Sh. trilioni 49.35, sawa na ongezeko la asilimia 11.2 kulinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24.
Ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia: Deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani; ajira mpya; ulipaji wa hati za madai; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; na maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwamo ujenzi na ukarabati wa viwanja.
Alisema mapato ya ndani - Serikali Kuu yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 33.254, misaada na mikopo nafuu kutoka washirika wa maendeleo Sh. trilioni 5.131 na mikopo ya kibiashara ndani na nje Sh. trilioni 9.604.
Kati ya Sh. trilioni 49.35 zinazotarajiwa kukusanywa na kutumika, matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa trilioni 34.590 na matumizi ya maendeleo Sh. trilioni 14.755.
MAONI YA WADAU
Wasomi, wanaharakati na wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu mapendekezo ya bajeti hiyo, wakisema ongezeko la kikokotoo litaongeza morali ya kazi, huku wakiwa na angalizo la kutegemea mikopo ya nje, kukosa mkazo wa kuwajengea wananchi uwezo wa kuzalisha na mwelekeo wa kijinsia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Dk. Damian Sambuo, alisema jana kuwa uamuzi wa serikali kusikiliza kilio cha wastaafu kuhusu malipo ya mkupuo ya kiinua mgongo utarejesha upya matumaini ya Watanzania katika uwajibikaji.
Alisema hatua hiyo inaleta mwanga mpya kwa watumishi wa umma na sekta binafsi. Ni kete kwa serikali kujenga morali ya watumishi wake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Dar es Salaam, Padri Dk. Francis Ngatingwa, alisema mwelekeo wa bajeti ya 2024/25, ni mzuri, lakini kuna shida anayoona ya kutegemea mikopo kutoka nje.
"Mwelekeo wa bajeti ni mzuri lakini suala la utekelezaji ni jambo jingine na wananchi tulitegemea ielezee mkakati wa namna ya kujenga barabara hususani za vijijini, ili wananchi waweze kupata unafuu kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni,”alisema.
Dk. Ngatingwa alisema zaidi ya Sh. trilioni 15 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa madeni ni fedha nyingi na itakuwa tatizo kama nchi itaendelea kukopa katika mwaka ujao wa fedha.
Mfanyabiashara Mohamed Kaburu alisema bajeti ya mwaka huu ni nzuri kutokana na kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa sukari nchini.
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Singida Mjini, Hassan Mboroo alisema ili kukabiliana na upungufu wa dola kuwekwe utaratibu wa kuuza bidhaa za nchini kwa fedha ya Tanzania badala ya fedha za kigeni ambazo zinasababisha kupunguza thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Gema Akilimali Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesema mapendekezo ya bajeti hayana mtazamo wa kijinsia kwa kuwa hayajaonesha kwa uwazi mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazokumba wanawake na watoto nchini.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Mafunzo wa TGNP, Anna Sangai, alisema walitegemea kusikia bajeti ikizungumzia uboreshwaji eneo la kilimo kwa ajili ya kukomboa wakulima ambao wengi ni wanawake kwa kuboresha teknolojia ya kisasa ya matrekta ili kuwainua kiuchumi.
Alishauri wabunge wanaojadili bajeti hiyo waitake serikali kuangalia namna itakavyowezesha wakulima wanawake vifaa vya kisasa vya kilimo ili kupambana changamoto zinazodhorotesha uzalishaji chakula.
*Imeandikwa na Romana Mallya (DAR), Godfrey Mushi (MOSHI), Thobias Mwanakatwe (SINGIDA) na Jenifer Gilla (DAR).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED