Katibu wa CHAWANYATA Temeke, na wenzake watuhumiwa kuvunja na kuiba

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 02:59 PM Mar 15 2024
Watuhumiwa wakiwa chini ya ulinzi wa askari kwa ajili ya kuingia mahakamani.
Picha: Imani Nathaniel
Watuhumiwa wakiwa chini ya ulinzi wa askari kwa ajili ya kuingia mahakamani.

Watuhumiwa sita akiwemo Katibu wa Chama cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania (CHAWANYATA) Wilaya ya Temeke, Michael Kateka (68) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke Dar es Salaam mapema leo wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuvunja na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 31.

Washtakiwa Wengine ni Bilali Juma(32) Mkazi wa Mtoni na wakazi wa Magurumbasi ni Isiaka Kapemba(32),Hemed Kapemba(32),  Fadhili Kapemba na mjumbe wa shina wa maeneo hayo,Hassan Kitigi.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Nicas Kihemba, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ally Mkama.

Wakili Kihemba alidai katika shtaka la kwanza inadaiwa kati ya Novemba 2,2022 maeneo ya Keko Makurumbasi washtakiwa kwa  pamoja walivunja  na kuingia kwenye duka la Isack Mtenga.

Aidha Katika shtaka la pili inadaiwa tarehe na maeneo hayo washtakiwa kwa pamoja waliiba vitu mbalimbali vya dukani ikiwemo tairi saba za gari,vioo vya gari vya scania,dawa za ng'ombe ,nyaraka mbalimbali pamoja na spana moja mbavyo vina  jumla ya  thamani  zaidi ya Sh milioni 31.

"Upelelezi umekamilka na ameiomba Mahakama hiiipange tarehe ya kuwasimea hoja za awali washtakiwa hao,"alidai Kihemba.

Washtakiwa hao walikana kutenda makosa hayo na kuomba dhamana.

Hakimu, Mkama alisema washtakiwa hao dhamana ipo wazi Kila mshtakiwa natakiwa awe na wadhamini wawili wawe na barua zinazotambulika kati ya hao mmoja anatakiwa atoe fedha taslimu kiasi cha Sh milioni 5 au hati yenye thamani hiyo na asaini bondi ya Sh milioni 5.

Washtakiwa wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na wamerudishwa  hadi kesho kwa ajili ya kupata dhamana.