JKCI yaanzisha huduma mpya kutibu wagonjwa moyo nyumbani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:11 AM Apr 24 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge.
PICHA: MAKTABA
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge.

TAASISI ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha huduma mpya ‘Home Based Care’ kwa wagonjwa wa moyo wa nyumbani ambao watawekewa shuka maalum lenye kifaa kitakachotoa taarifa moja kwa moja hospitalini za mapigo ya moyo, umeme wa moyo na hali ya presha kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, akifafanua kuwa, shuka hilo maalum litakuwa na kifaa kitakachowezesha wataalam walioko JKCI kupata taarifa za mgonjwa aliyeko nyumbani moja kwa moja.

Dk. Kisenge ambaye ni Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, amesema mgonjwa akihitaji huduma ya saa 24 akiwa nyumbani atapewa kupitia daktari au nesi.

Amesema kupitia huduma hiyo watawahudumia wagonjwa wakiwa nyumbani hususani waliokuwa wamelazwa JKCI na kuruhusiwa, lakini bado wanahitaji uangalizi maalum.

“Wakiwa nyumbani tutaendelea kuwahudumia. Tumekuja na huduma mpya kabisa ya teknolojia ya juu ambapo mgonjwa atalalia shuka maalum na kuweka kifaa maalum chini ya kitanda chake na sisi tutaweza kugundua mapigo ya moyo au umeme wa moyo na tutagundua presha zake zikoje.

“Tutaweza kujua oksijeni yake ikoje kwa kuwa wagonjwa waliozidiwa sana presha hushuka ghafla na kupoteza maisha. Akiwa nyumbani tutapata ujumbe kwamba mgonjwa yupo nyumbani na presha zimeshuka na itakuwa rahisi kumfuata aliko,” amesema.

Dk. Kisenge amesema JKCI ina magari ya wagonjwa zaidi ya sita, wanaweza kumfuata mgonjwa na kumpeleka hospitalini hapo na kumhudumia.

Kupitia teknolojia hiyo mpya ambayo inatumika nchini India, wanaweza kumwambia ndugu nini cha kufanya.

“Mgonjwa anakuwa na kitanda chake tunamwekea hicho kitambaa kitakuwa kinapima mapigo ya moyo, presha na oksijeni akiwa nyumbani. Tutawahudumia wagonjwa waliozidiwa kwa kuwafuata waliko. Jamii imekuwa na watu wazima kuwaleta inakuwa shida.

“Akituambia tutamfuata aliko na kumpa huduma kwa madaktari au nesi kwenda, lakini wengine wamefanyiwa operesheni wanakuwa na vidonda wanahitaji kusafishwa, nesi wanaweza kwenda kumsafisha,” amesema.

Dk. Kisenge amesema kuna wagonjwa waliokaa hospitalini kwa muda mrefu wanahitaji huduma wakiwa na ndugu zao nyumbani, hivyo JKCI itaitoa kwa madaktari au nesi kwenda kumhudumia.

“Kupitia hivi vifaa sisi tutaona mgonjwa wetu anaendeleaje kule nyumbani,” amesema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dk. Smitha Bhalia, amesema; “Kama mgonjwa atabadilika ghafla na kuhitaji uangalizi daktari kumwona, atamfuata na kuangalia kama anahitaji kuletwa hospitalini au kuandikiwa tu dawa na kubaki nyumbani.”

 Dk. Smitha ameongeza kuwa, “Mfano wagonjwa waliopooza au waliofanyia operesheni ya moyo na kuhitaji mazoezi ya viungo wanaweza kuyapata akiwa nyumbani.

Vilevile, kwa wagonjwa wenye shida ya kupungua au wenye uzito mdogo wanahitaji mtaalam, atamfuata nyumbani na kumwelezea vyakula anavyostahili kula.